chollo |
MWADUI wameamua, kama
ulidhani ni Yanga, Simba na Azam pekee ndizo zinatisha huko sokoni basi
umeingia 'chaka', klabu ya Mwadui FC leo imefanya balaa baada ya kuwashusha
mgodini nyota takribani wanane wakiwemo wapya na wa zamani.
Taarifa kutoka chanzo chetu ndani ya wazee hao wa mgodini ni
kwamba beki wa Kagera Sugar, Salum Kanoni tayari amesaini mkataba wa mwaka
mmoja kujiunga na Mwadui sawa na Said Nassor 'Chollo' ambaye msimu uliopita
alikuwa Stand United.
Kanoni alipoulizwa sababu iliyomfanya aachane na Kagera
alisema "Nimekuwa ndani ya Kagera kwa kipindi kirefu sana, nadhani sasa
nahitaji changamoto mpya ndio sababu nimeona nije Mwadui."
Beki Joram Mgeveke ambaye alikuwa klabuni hapo kwa mkopo
akitokea Simba SC, amemaliza mkataba wake na wekundu hao na 'fasta' Mwadui
wamemweka chini huku taarifa zikisema kuna uwezekano mkubwa akawa amesaini
mkataba leo sambamba na kiungo Hassan Kabunda na beki Iddy Moby ambao wanaongezewa
mikataba klabuni hapo.
Wakati huo huo kiungo wa Toto African, Abdallah Seseme yupo
Shinyanga na atamalizana na Mwadui muda wowote kwavile mazungumzo yao
yameshafikia pazuri.
Mwadui pia iko mbioni kuvunja ukuta wa Coastal Union kwa
kumalizana na walinzi Abdallah Mfuko na Adeyum Saleh huku pia David Luhende na
Kevin Sabato wakionekana katika maeneo ya kujidai ya wachimba madini hao
kuashiria kuna 'dili' ya kuongezewa mikataba.
CHANZO: BOIPLUS
Post a Comment