MSHAMBULIAJI wa timu ya Yanga, Amissi Tambwe,amesema
amemaliza bifu na Donald Ngoma na kuahidi kutoa ushirikiano utakaowezesha timu
hiyo kupata pointi tatu katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya
Medeama ya Ghana.
Nyota hao tegemeo katika safu ya ushambuliaji ya Yanga
walipigana wakati timu ikiwa kambini nchini Uturiki na kuwekeana bifu, hali
iliyomfanya kocha Hans van der Pluijm kuingilia kati ili kusuluhisha ugomvi
wao.
Akizungumza jana, Tambwe ambaye aliumizwa vibaya na
kukimbizwa hospitalini kwa matibabu, alisema amemsamehe Ngoma na sasa anaungana
naye ili kusaidia ushindi dhidi ya Medeama watakaovaana Juni 16, mwaka huu
katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Ugomvi wetu umekwisha sasa sina tatizo na Ngoma kwa sababu
ni mchezaji mwenzangu ambaye tutashirikiana kwa pamoja kusaka ushindi katika
mchezo dhidi ya Medeama ili kujiwekea mazingira mazuri zaidi. “Mashabiki
waondoe wasiwasi maana nafikiri jambo hili liliwaumiza sana na walikuwa
wanasubiri kwa hamu kusikia tumefikia mwafaka, kwa sasa tutacheza kwa
ushirikiano wa hali ya juu ili tufikie malengo yetu,” alisema Tambwe.
Ugomvi wa mastraika hao ulipokelewa kwa hisia tofauti na
mashabiki wa Yanga,kutokana na kutokea kipindi ambacho timu inakabiliwa na
mechi ngumu za kimataifa na ushirikiano wao uwanjani ni muhimu.
Post a Comment