KIPA wa zamani wa timu ya taifa ya Ivory Coast, Daniel Techi
Yeboah, ametua nchini jana jioni tayari kabisa kuanza majaribio kesho ya
kujiunga na mabingwa wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup),
Azam FC.
Yeboah mwenye umbo kubwa la kimpira na urefu wa wastani
anaungana na kipa kutoka Hispania, Juan Jesus Gonzalez, ambao wote wataanza
kujaribiwa katika mazoezi ya Azam FC ya kujiandaa na msimu ujao yaliyoanza leo Alhamisi.
Kipa huyo aliyekuwa akikipiga katika timu ya KSV Oostkamp ya
Ubelgiji, amewahi pia kukipiga nchini Ufaransa ndani ya vikosi vya Bastia na
Dijon huku akianzia soka lake kwa miamba ya Ivory Coast, Asec Mimosa’s.
Wakati akiwa Mimosas, aliwahi kuwa nahodha wa beki kisiki wa
kati wa Azam FC, Pascal Wawa kabla ya beki huyo kutimkia kwa miamba ya Sudan,
El Merreikh, pia amewahi kufanya kazi na kipa wa Simba, Vincent Angban, ambaye
alifanikiwa kumweka benchi na kisha kutimkia Ufaransa.
Yeboah pia amewahi kuchezea kikosi cha timu ya Taifa ya
Ivory Coast kilichoshiriki Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini mwaka 2010 na
fainali za Mataifa ya Afrika 2013 nchini humo, kilichoundwa na mastaa wengine
kama vile Didier Drogba, Didier Zokora, Kolo Toure, Yaya Toure, Solomon Kalou,
Aruna Dindane, Emmanuel Eboue.
Akizunguma baada ya kuwasili nchini jana na kupokelewa na
Meneja wa Azam FC, Luckson Kakolaki, Yeboah alisema kuwa amekuja akiwa na fiti
na kazi yake ni moja tu kuhakikisha anashinda changamoto zote na kusajiliwa na
timu hiyo.
“Kwanza siku zote mimi huwa napenda sana upinzani na
nimekuja hapa nikiwa kamili kukaniliana na hilo, mashabiki watafurahi wenyewe
nikifanikiwa kubaki hapa,” alisema.
Baadhi ya dondoo za kiwango chake, ni uwezo wake mkubwa wa
kuzuia michomo, kuusoma mchezo pamoja na mawasiliano mazuri na walinzi wake
akiwa langoni, ambapo kutokana na kipaji chake cha hali ya juu aliwahi
kufananishwa na gwiji wa zamani wa Ivory Coast, Alain Gouamene.
Post a Comment