HATIMAYE Simba imeamua kutegua kitendawili na kukiri kuwa
msimu ujao hawatakuwa na mshambuliaji Mganda, Hamis Kiiza na tayari
wamemalizana kwa amani.
Tangu kumalizika kwa Ligi Kuu Bara 2015-16, kumekuwa na
taarifa mbalimbali juu ya kutemwa kwa mshambuliaji huyo kutokana na sababu za
utovu wa nidhamu lakini hakukuwa na kiongozi aliyewahi kuthibitisha kuhusiana
na hilo zaidi ya kutoa kauli zenye viashiria vya hali kama hiyo.
Aidha, ilielezwa kuwa Kiiza anaweza kutemwa pamoja na Mganda
mwenzie, Juuko Murshid kutokana na kufuata mkumbo wa kugoma kuichezea timu hiyo
mpaka wapewe mishahara yao.
Rais wa Simba, Evans Aveva ameliambia Championi Jumatatu kuwa
sasa ni rasmi wameshampa Kiiza mkono wa kwaheri na hakuna tena kilichopo baina
yao na zaidi wamemtakia kila la kheri huko aendako pamoja na kumshukuru kwa
mchango wake mkubwa alioutoa kwa timu hiyo msimu uliopita.
“Niseme tu kwamba tumemalizana kistaarabu kabisa na Kiiza na
tunamtakia mema, kila la kheri huko aendako lakini pia kwa kweli tunamshukuru
kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa Simba msimu uliopita,” alisema Aveva.
Kiiza aliyewahi kuichezea Yanga anaungana na wachezaji
wengine wa kigeni waliotemwa msimu huu klabuni hapo; Mkenya, Raphael Kiongera,
Mrundi, Emiry Nimubona na Mganda, Brian Majwega.
Post a Comment