CHIRWA |
WALE waliokuwa
wanabeza kiwango cha mshambuliaji mpya wa Yanga Mzambia, Obrey Chirwa jiandaeni
kupata aibu, baada ya Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm kuona mabadiliko
makubwa ya ndani ya uwanja kwa nyota huyo huku akiahidi watamuelewa.
Kauli hiyo
aliitoa Pluijm mara baada ya mshambuliaji huyo kupiga bonge la bao kwa njia ya
kichwa akiunganisha krosi ya Simon Msuva kwenye mazoezi ya Ijumaa iliyopita
yaliyofanyika Uwanja wa Boko Beach Veterani jijini Dar es Salaam.
Mshambuliaji
huyo, kiwango chake kilibezwa na baadhi ya mashabiki wa timu hiyo mara baada ya
mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe mchezo uliopigwa kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar.
Pluijm ameliambia
gazeti hili kuwa ameona mabadiliko makubwa ya mshambuliaji huyo ikiwemo
kuendana na kasi ya wachezaji wenzake ndani ya uwanja kwa kucheza soka la pasi
za haraka wakati akiwa na mpira.
Pluijm alisema
tayari ameanza kushika mifumo na staili zote za uchezaji ambazo yeye anazitumia
katika kuhakikisha timu inapata ushindi kwenye mechi zao.
"Nimefurahishwa
na bao zuri la kichwa lililofungwa na Chirwa katika mazoezi ya leo (Ijumaa),
hiyo ni ishara tosha kuwa hivi sasa ameanza kubadilika kuendana na kasi ya soka
lile linalohitaji kama walivyokuwa wenzake.
"Kama
unavyojua Chirwa ni mgeni amejiunga na timu hivi karibuni, ilikuwa ni vigumu
kwake kushika mifumo, staili na kuendana na kasi na wenzake aliowakuta, hivyo
ni lazima aanze taratibu na baadaye aanze kuzoea," alisema Pluijm.
Wakati huohuo, kuonyesha sasa hataki masihara hata kidogo
wakati wanajiandaa kabla ya kuwavaa Medeama katika mchezo wa Kombe la Shirikisho
utakaopigwa wiki hii, Pluijm aliamua kuwapa adhabu washambuliaji wake, Donald
Ngoma na Chirwa mara baada ya kushindwa kupachika mabao mazoezini.
Katika mazoezi ya juzi Jumamosi, Ngoma, Chirwa na wachezaji
wengine isipokuwa Thaban Kamusoko pekee walipewa adhabu ya kupiga ‘push up’
mara baada ya kukosa mabao.
Pluijm alipanga mipira nje kidogo ya 18 na kuwataka wachezaji
wote kufunga lakini wengi wao wakawa wanapaisha na kujikuta wakipata adhabu
hiyo isipokuwa kwa Kamusoko pekee ambaye alifanya zoezi hilo vyema.
Pluijm alifungukia juu ya zoezi hilo ambapo alisema: “Tuna
tatizo la kufunga kama ulivyoona kwenye mechi mbili zilizopita hivyo ninachokifanya
ni kuwapa mbinu zaidi za kufunga siyo kwa washambuliaji bali timu nzima, nataka
kuona tunakuwa wazuri zaidi katika kumalizia nafasi tunazozitengeneza.”
Post a Comment