ILI kujenga nidhamu
ndani ya kikosi chao, Azam FC imeweka sheria ndogo ambayo mchezaji
atakayechelewa mazoezini atapigwa faini ya dola 50 ambazo ni sawa na Sh
107,168.
Azam ambayo juzi Alhamisi ndiyo imeanza
maandalizi ya msimu ujao, imepiga kambi kwenye hosteli zao zilizopo katika
uwanja wao wa Azam Complex jijini Dar.
Mara baada ya kumaliza mazoezi ya jana
asubuhi, kocha msaidizi wa kikosi hicho, Denis Kitambi aliwatangazia wachezaji
wote kuwahi uwanjani dakika 15 kabla ya kuanza kwa mazoezi ya jioni yaliyoanza
jana saa 9:00 jioni.
“Atakayechelewa lazima apigwe faini ya dola
50, si masihara kama kuna mtu atadhani utani basi achelewe ili aone
kitakachotokea,” alisema Kitambi.
Azam pia kupitia maagizo ya kocha wao mpya,
Zeben Hernandez itaanza mpango wa kurekodi vipindi vyote vya mazoezi kisha
baadaye vitakuwa vinapitiwa ili kutazama ufanisi wa kila mmoja wao.
“Nataka mazoezi yetu yarekodiwe picha za video
halafu baadaye natazama ufanisi wa kila mchezaji ili kukifanya kikosi kuwa bora
zaidi,” alisema Hernandez raia wa Hispania.
Hernandez pia ametoa siku 15 za kuangalia
uwezo wa wachezaji wake kabla hajatangaza jeshi lake la msimu ujao.
Post a Comment