Bukungu wa kwanza kulia

BEKI wa zamani wa TP Mazembe anayewania nafasi ya kusajiliwa Simba, Besala Janvier Bukungu amesema anamjua vizuri straika wa Yanga, Donald Ngoma na mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi watulie kwani atamtuliza.
Pia Bukungu alisema amepata taarifa kwamba Simba anayotaka kujiunga nayo msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara ilifungwa mara mbili na Yanga, kisha akatikisa kichwa.
Bukungu raia wa DR Congo amesikitishwa na vipigo hivyo vya mabao 2-0, papo hapo akaliambia Championi Jumamosi kwamba: “Lazima tulipe kisasi na naahidi mashabiki wa Simba hawatalia tena.”
Beki huyo anayemudu kucheza nafasi zote za beki iwe kulia au katikati, alisema amepewa taarifa kwamba mara zote ambazo Simba imefungwa na Yanga, mashabiki wake walikuwa wakiangua vilio, hivyo amewaambia sasa basi imetosha.
Bukungu mrefu na mwenye mwili mkubwa alisema anaamini kama mambo yakienda sawa na akasajiliwa na Simba, hawatakubali kufungwa tena na Yanga. 
Ngoma

Beki huyo tayari amejiunga na Simba na kuanza mazoezi ya pamoja chini ya kocha mpya raia wa Cameroon, Joseph Omog aliyetua wiki iliyopita na kusaini mkataba wa miaka miwili ya kukinoa kikosi hicho.
“Wanasimba wajiandae kufurahia kwenye msimu ujao na siyo vilio kila walipokuwa wanakutana na Yanga kisha kufungwa, nitashirikiana na wenzangu kuwapa furaha mashabiki wa Simba,” alisema Bukungu.
Bukungu ambaye aliwahi kuichezea timu ya taifa ya DR Congo na klabu kubwa za TP Mazembe na Esperance ya Tunisia, alisema: “Nimesikitishwa na taarifa za Yanga kuifunga Simba mara zote walizokutana kwenye ligi kuu, kiukweli nimeumizwa nazo na niwaahidi Wanasimba kuwa ni lazima tulipe kisasi kwa staili yoyote.
“Hakuna kisichoshindikana kwangu, mimi kama beki nitatimiza wajibu wangu wa kutokubali kuruhusu bao liingie golini kwetu, hivyo nitapambana kuhakikisha tunawafunga Yanga kila tutakapokutana nao,” alisema Bukungu.
“Niwaambie tu mashabiki wa Simba kuhusu straika wa Yanga anaitwa Ngoma, namjua na nimewahi kukabana naye katika mechi za timu za taifa, yeye akiwa Zimbabwe mimi DR Congo.
“Siyo mtu anayetisha sana, ila inatakiwa umakini kumzuia na mimi nitaifanya hiyo kazi kama mambo yakienda vizuri halafu utaona kama Simba itafungwa tena na Yanga,” alisema Bukungu.
Naye kiungo mshambuliaji raia wa DR Congo, Mousa Ndusha anayewania kusajiliwa Simba, alisema: “Ni bora tufungwe na Azam FC ambayo naamini wanacheza soka safi na la kuvutia lakini siyo Yanga.
“Yanga niliwaona wakicheza na TP Mazembe, siyo timu ya kuiogopa na inafungika.”

Post a Comment

 
Top