SIMBA
imefanya tukio moja la kimafia kidogo, kwani ilimsafirisha straika Ndjack Anong
Guy Seuges raia wa Cameroon usiku kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ilipo
kambi yake na jana asubuhi akaonekana mazoezini.
Hakuna mchezaji wa Simba aliyefahamu ujio wa straika
huyo zaidi ya asubuhi kumuona wapo naye mazoezini na kuzua maswali vichwani
mwao lakini wakaambiwa: “Huyu kaja kujaribiwa.”
Mmoja wa wachezaji wa Simba waliopo kambini Chuo cha
Biblia cha Highlands, Morogoro alisema kuwa: “Hadi usiku tunalala hatukuwa
tunafahamu kama kuna mchezaji anakuja, lakini asubuhi tukashtukia mtu mpya
mazoezini.”
Mmoja wa mabosi wa Kamati ya Usajili ya Simba ambaye
hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema: “Ujio wa Mcameroon huyu ni
mwendelezo wa kusaka wachezaji, atafanyiwa majaribio kuona kama anafaa.”
Kocha Joseph Omog na msaidizi wake Jackson Mayanja walimpokea Seuges
na kuanza kutazama uwezo wake na watatoa majibu siku chache zijazo. Mayanja alikiri
kumpokea Seuges.
Seuges ameungana na wachezaji wengine wa kigeni
wanaowania kusajiliwa Simba wakiwemo Musa Ndusha na Janvier Bukungu (wote
kutoka DR Congo), Muivory Coast, Blagnon Fredric na Mzimbabwe, Method Mwanjali.
“Kwa jinsi ninavyowaona wote wanaweza kubakia kwa sababu
wanaonyesha uwezo mzuri uwanjani lakini jibu kamili tutalijua kesho (leo) au
keshokutwa (kesho) Jumapili baada ya makocha kumaliza kazi yao,” alisema bosi
huyo wa Simba.
Post a Comment