HAINAGA
ushemeji, Yanga inakulaga Medeama, ndiyo wimbo utakaoimbwa na mashabiki wa
Yanga leo Jumamosi wakati timu yao itakapokuwa ikipambana na Medeama ya Ghana
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika kuhakikisha wanarejesha morali ya timu na
kuwafariji mashabiki hao, Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm
ameapa kuwa ni lazima wawafunge Medeama ili mbele mambo yao yawe safi.
Yanga inacheza na Medeama mechi ya Kundi A ya Kombe la
Shirikisho Afrika, ambayo itaonyeshwa moja kwa moja na Azam TV.
Yanga inahitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri
ya kutinga nusu fainali ya michuano hiyo kwani ipo mkiani mwa kundi hilo ikiwa
haina pointi huku TP Mazembe ikiwa kileleni na pointi sita.
Katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi A, Yanga ikiwa
ugenini ilifungwa na MO Bejaia ya Algeria bao 1-0, halafu ikafungwa tena bao
1-0 na TP Mazembe Juni 28, mwaka huu hapa nchini.
Pluijm alisema maandalizi makubwa aliyoyafanya ya wiki
mbili yanatosha kabisa timu yake kupata ushindi kwenye mechi na Medeama.
Pluijm alisema tayari amewaona wapinzani wao kupitia
video mbalimbali za mechi zao na kikubwa alichokiona Medeama wana fiziki ya
kutosha, hivyo ni lazima aanzishe wachezaji wapambanaji.
Mholanzi huyo alisema, katika mechi hiyo anataka kuona
kila nafasi watakayoipata ya kona, faulo na krosi wanaitumia vizuri kwa kufunga
mabao ili kuhakikisha wanashinda mechi.
“Mechi yetu na Medeama ya kesho (leo) tutapambana kufa
na kupona kuhakikisha tunapata ushindi ili saikolojia ya wachezaji wangu irejee
kutokana na presha waliyonayo wakihitaji ushindi.
“Ninashukuru morali ya wachezaji wangu ipo juu na
maandalizi niliyoyafanya yanatosha kutupa ushindi, najua siyo kazi rahisi,
lakini tutapambana kuhakikisha tunawafunga Medeama.
“Kutokana na makosa ya safu yangu ya ushambuliaji kwenye
mechi mbili tulizofungwa, nimeifanyia marekebisho kwa kuwapa mbinu mbalimbali
washambuliaji wangu.
“Nimewapa mbinu za kucheza kona, faulo na krosi, hivyo
nimewataka wachezaji wangu kutumia kila nafasi tutakayoipata kwa ajili ya
kufunga bao,” alisema Pluijm.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alisema:
“Sisi tupo vizuri na hatutaki kuwaangusha tena mashabiki
wetu, waje uwanjani wapate furaha.”
Kwenye mazoezi yao ya jana jioni kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar, Medeama walizuia kupigwa picha huku wakionekana kuwa na hofu.
Kocha wa Medeama, Prince Owusu, alisema: “Naijua Yanga
vizuri, tumekuja kupambana kwani wote bado tuna nafasi ya kuingia nusu fainali,
sitarajii mchezo rahisi na wala Yanga isitarajie urahisi.”
Nahodha wa Medeama, Mohammed Tagoe, alisema wamekuja
kushindana na kama wanabezwa ukweli utadhihirika uwanjani.
Kutokana na mazoezi ya Yanga ya jana asubuhi kwenye
Uwanja wa Boko Veterani, Dar, kikosi chao kinaweza kupangwa hivi: Deogratius
Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Vincent Bossou, Mbuyu
Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Obrey
Chirwa.
Post a Comment