BEKI wa Yanga, Juma Abdul Jaffar Mnyamani ameshinda tuzo ya
Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2015/2016.
Katika sherehe za utoaji wa tuzo hizo usiku huu ukumbi wa
Double Tree Hotel By Hilton, Masaki, Dar es Salaam, Abdul ambaye pia ni
mchezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars amewashinda beki mwenzake, Mohammed
Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba na kiungo wa Mtibwa Sugar, Shizza Kichuya.
Na kwa ushindi huo, Abdul mbali na kukabidhiwa taji na mgeni
rasmi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, pia atazawadiwa fedha Sh
Milioni 9.2 wakati klabu yake, Yanga SC itazawadiwa Sh. Milioni 81.3 kwa kuwa
bingwa, huku Sh. Milioni 40.6 zikienda kwa washindi wa pili, Azam FC, Sh
Milioni 29 zikienda kwa washindi wa tatu, Simba SC na Sh. Milioni 23.2 zikienda
kwa Prisons washindi wa nne.
Aishi Salum Manula wa Azam FC ameshinda tuzo ya kipa Bora
akiwaangusha Deo Munishi ‘Dida’ wa Yanga na Benno Kakolanya wa Prisons na
kuzawadiwa Sh. Milioni 5.7 huku mfungaji bora Amissi Tambwe wa Yanga
akizawadiwa pia Sh. Milioni 5.7.
Thabani Michael Kamusoko ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa
Kigeni, akiwaangusha Mzimbabwe mwenzake anayecheza naye Yanga SC, Donald Ngoma
na kipa Muivory Coast wa Simba, Vincent Agban hivyo kuzawadiwa Sh. Milioni 5.7
pia.
Mholanzi Hans van der Pluijm ameshinda tuzo ya Kocha Bora na
kuzawadiwa Sh. Milioni 8, akiwaangusha Mecky Maxime wa Mtibwa Sugar na Salum
Mayanga wa Prisons.
Tshabalala ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi
akiwaangusha Farid Mussa wa Azam na Shizza Kichuya wa Mtibwa Sugar na
kuzawadiwa Sh. Milioni 4.
Ibrahim Hajib wa Simba ameshinda tuzo ya Bao Bora la Msimu
na kuzawadiwa Sh. Milioni 3 akimuangusha Tambwe wa Yanga, wakati Mtibwa Sugar
imezibwaga JKT Ruvu na Mgambo Shooting katika tuzo ya Timu yenye Nidhamu na
kuzawadiwa Sh. Milioni 17.2.
Ngole Mwangole ameshinda tuzo ya Refa Bora na kuzawadiwa Sh.
Milioni 5.7 baada ya kuwaangusha Anthony Kayombo na Rajab Mrope.
Post a Comment