ILE ishu ya beki wa Yanga, Hassan Kessy ya kuzuiwa kuanza
kuitumikia timu yake hiyo mpya katika mechi mbalimbali za kimashindano,
inatarajiwa kutolewa ufumbuzi leo Jumatatu.
Kessy aliyejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili
akitokea Simba, tangu ajiunge na timu hiyo miezi miwili iliyopita, hajaicheza
hata mechi moja timu hiyo kutokana na Simba kumwekea ngumu ikidai haijamalizana
naye.
Hivi karibuni iliripotiwa kwamba, ili Simba imuachie Kessy
aanze kuichezea Yanga, basi Wanajangwani hao wanatakiwa kutoa kitita cha zaidi
ya Sh milioni 126, pesa ambazo Yanga haitaki kuzitoa kwa kile walichodai kabla
hawajamsajili mchezaji huyo, alikuwa amemaliza mkataba wa kuitumikia Simba.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasoka wa Kulipwa Tanzania
(Sputanza), Mussa Kisoky amesema kuwa leo ndiyo watakuwa na majibu kamili juu
ya sakata hilo ambalo limeteka hisia za wengi.
“Baada ya kupata malalamiko kutoka upande wa mchezaji,
tukawasilisha malalamiko hayo TFF (Shirikisho la Soka Tanzania), lakini kesho
(leo Jumatatu) ndiyo nitakuwa na majibu kamili juu ya nini kitafuatia,
ukinitafuta mchana nitakwambia itakavyokuwa,” alisema Kisoky.
Wakati huohuo, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema
kuwa, ishu hiyo imekwama sehemu moja tu ambapo ni upande wa Yanga uliotakiwa
kuandika barua, lakini wamekuwa wagumu kufanya hivyo wakihofia kujiingiza
kwenye mtego wa kulipa hizo Sh milioni 126.
Post a Comment