SASA ni asilimia zaidi ya 80
mshambuliaji Kipre Herman Tchetche hatarejea nchini kuitumikia Azam FC kwa kuwa
amegoma kurejea.
Tchetche, raia wa Ivory Coast,
inaelezwa yuko nyumbani kwao ambako ameamua kubaki na kukataa kujiunga na kambi
ya Azam FC hali ambayo imezua hofu na kuunganisha kwamba mabingwa wa Tanzania,
Yanga wamemficha.
Mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye
hakutaka kutajwa jina, amesema hivi: “Kweli Kipre ni mchezaji bora, kama
tukimhitaji basi tunajua cha kufanya. Ila si wakati mwafaka kulizungumzia, kama
hajarudi Azam, hilo ni yeye na timu yake.”
Hata hivyo, Azam FC wanaonekana
kutokuwa na hofu kwa kuwa mchezaji huyo amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na
timu hiyo ya Chamazi na kocha mpya, Zeben Hernandez amekuwa akisisitiza kwamba
anamhitaji.
“Kuna hofu kuwa kuna timu inamrubuni
Kipre, uongozi wa Azam FC uko imara kwa kuwa ana mkataba wa mwaka mmoja,
watajisumbua tu,” kilieleza chanzo kutoka ndani ya Azam.
Rafiki wa karibu wa Kipre ameliambia
gazeti hili kuwa Tchetche alizungumza na mmoja wa mabosi wa Azam FC na kusema
ameshindwa kuja kwa kuwa aliuziwa nyumba kwao Ivory Coast lakini kuna harufu ya
utapeli.
“Baada ya juhudi za kumpata kwa zaidi
ya wiki, juzi alipatikana akazungumza na mmoja wa mabosi na kusema anachelewa
kwa kuwa alitapeliwa katika mauzo ya nyumba, hivyo hadi alimalize suala hilo na
hatujui ni lini,” kilifafanua zaidi chanzo.
Tayari Azam FC imeanza maandalizi ya
msimu mpya chini ya Hernandez na jopo lake na kocha huyo ameusisitiza uongozi
kufanya juu chini kumrejesha kundini.
Kuhusu Yanga kumhitaji, wakati fulani
Kocha Hans van Der Pluijm aliwahi kusema wazi kwamba angependa kuwa naye katika
kikosi chake.
Yanga kushindwa kuonyesha cheche
katika michuano ya kimataifa hasa katika safu ya ushambuliaji chini ya Donald
Ngoma, Amissi Tambwe na Obey Chirwa, inaweza kuchangia Yanga kufanya juu chini
kumpata kwa kuwa ina michuano ya Ligi ya Mabingwa, msimu ujao.
Alipoulizwa kuhusiana na hilo jana,
Msemaji wa Azam FC, Jaffar Iddi alisisitiza hivi: “Kipre ana mkataba na Azam,
kama kuna timu inamhitaji inakaribishwa na uongozi. Suala la amefika au atafika
lini, litafuata baadaye.”
Taarifa nyingine zinaeleza, Kipre
ameingia katika hali ya kutoelewana na mmoja wa viongozi wa Azam FC, hali
ambayo inamfanya aone Yanga ni sehemu sahihi kwenda.
Kama ataendelea kuchelewa, Azam FC
imesisitiza itamwadhibu na kama anataka kuuzwa, vema akaiambia klabu. Kocha
Hernandez licha ya kumtaka, naye amechukua tahadhari kuanza kutafuta
mshambuliaji mpya wa uhakika hasa iwapo, ishu ya kumrejesha itakwama kwa
asilimia 100.
Tayari wachezaji kadhaa wa kimataifa
wamekuwa wakipishana kufanya majaribio katika kikosi hicho.
Post a Comment