MABINGWA wa zamani wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, Mtibwa Sugar ya Morogoro wamemsajili mshambuliaji wa Mwadui FC
ya Shinyanga, Rashid Mandawa.
Mratibu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser amesema
mbali na mshambuliaji huyo wa zamani wa Kagera Sugar, pia wamemsajili beki wa
kati Cassian Ponera kutoka Ndanda FC ya Mtwara.
Bayser pia amesema wamefanikiwa kuwaongezea
mikataba wachezaji wao kadhaa wakiwemo kipa Said Mohamed na beki wa kati Salim
Mbonde.
"Usajili unaendelea kwa umakini mkubwa
chini ya Mwalimu Salum Mayanga kuziba mapengo hususan kwenye eneo la kiungo
ambako tumeondokewa na Mzamiru Yassin, Mohamed Ibrahim na Shiza Kichuya ambao
wote wameenda Simba,"amesema Bayser.
Mabigwa hao wa 1999 na 2000 wa Ligi Kuu,
wanatarajiwa kuanza rasmi mazoezi Jumatatu hii kujiandaa na msimu mpya.
Bayser amesema kambi ya mazoezi itaanzia
Dar es Salaam kabla kuhamia makao makuu ya timu, Manungu, Turiani mkoani
Morogoro wiki moja baadaye.
Post a Comment