MSHAMBULIAJI
wa Yanga, Mzambia, Obrey Chirwa, ametamka kuwa mashabiki wa timu hiyo
wanatakiwa kumpa muda kwa ajili ya kuendelea kuzoea mazingira ndani ya kikosi
hicho kabla ya kuonyesha makali yake ambayo yalilifanya benchi la ufundi la
timu hiyo kumsajili.
Chirwa
mpaka sasa amefanikiwa kushuka dimbani kuichezea timu hiyo mara mbili katika
michezo baina ya TP Mazembe na Medeama ya Ghana lakini katika michezo yote hiyo
ameshindwa kufunga bao lolote.
Katika mchezo
wa juzi dhidi ya Medeama, Chirwa alikosa nafasi nyingi za wazi na kupata lawama
nyingi kutoka kwa mashabiki wa Yanga kwenye mchezo huo uliomalizika kwa sare ya
bao 1-1 na kuiweka Yanga katika mazingira magumu zaidi ya kusonga mbele.
Chirwa
ambaye ametokea Klabu ya FC Platinum ya Zimbabwe, aliyotokea mshambuliaji
mwingine wa timu hiyo, Donald Ngoma na kiungo Thaban Kamusoko, amesema kuwa,
licha ya mashabiki wa timu hiyo kuendelea kumlaumu kutokana na kushindwa
kuibeba timu hiyo, kwa upande wake anaomba wampe muda kabla ya kuonyesha
thamani yake.
“Siyo
kama nashindwa kufanya vyema, bado naendelea kujifunza mambo mengi ndani ya
timu na hata kama unavyoona nakuwa napambana kwa uwezo wangu wote kuisaidia
timu lakini mambo tu ndiyo yanakuwa tofauti, lakini kikubwa ambacho nawaomba
mashabiki wa Yanga, ni kwamba waendelee kuwa wavumilivu kabla ya mambo kuwa
mazuri hapo baadaye.
“Sijaona
tatizo lolote kwetu licha ya mpaka sasa kutofanikiwa kushinda mchezo wowote ule
katika Kombe la Shirikisho. Naamini bado tuna nafasi ya kufanya vyema kama
tukijipanga katika michezo ijayo kwani hatujakata tamaa na imani yetu ni kwamba
tuna nafasi ya kutinga nusu fainali,” alisema Chirwa.
Post a Comment