JOSEPH Omog hataki utani hata kidogo, anataka kutengeneza kikosi cha ubingwa, tayari inaelezwa amewatema nyota wawili raia wa Congo waliokuwa wakifanya majaribio kwa siku kadhaa klabuni hapo.
 Nyota ambao inaelezwa kocha huyo wa Simba raia wa Camaroon amewakataa ni Musa Ndusha na Janvier Bukungu lakini Blagnon Fredric raia wa Ivory Coast na Mzimbabwe, Method Mwanjali pamoja na Mcameroon, Ndjack Anong Guy Seugesakiwa, bado wanaendelea kuangaliwa zaidi katika majaribio.
Simba kwa sasa imeweka kambi mkoani Morogoro huku ikiwa inawafanyia majaribio wachezaji kadhaa kutoka sehemu mbalimbali ili kuhakikisha inakuwa na kikosi bora kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Bosi kutoka ndani ya Klabu ya Simba ambaye hakutaka jina lake liwekwe wazi, alifunguka kuwa, Omog amefikisha taarifa kwa uongozi wa klabu hiyo kuwa hajaridhishwa na viwango vya wachezaji hao, hivyo anahitaji wengine zaidi aweze kuwaangalia.
Hata hivyo, Omog ameonekana kukazania zaidi mazoezi ya fiziki kwa wachezaji wake ili kuwaongezea stamina ikiwa ni pamoja na kuchunguza uwezo wa kila mmoja.
“Kocha hajakubaliana na viwango vya wachezaji wote Wacongo wanaofanya majaribio, hivyo anahitaji wachezaji wengine zaidi kwa ajili ya kuwapima.
“Kufuatia taarifa hiyo, kuna wachezaji wengine zaidi wanatarajiwa kutua kuanzia wiki ijayo ili kuweza kuona ni wachezaji gani ambao watakuwa na viwango ili waweze kusajiliwa na kuna mazungumzo yanaendelea na wachezaji mbalimbali.
“Wachezaji watakaotua watakuja kuangaliwa zaidi katika mechi yetu ya kirafiki ya Simba Day ambayo tutacheza tarehe nane mwezi ujao,” alisema bosi huyo.

Post a Comment

 
Top