ZAIDI ya asilimia
90, Azam FC inataka kuachana na fowadi wao, Kipre Tchetche, kutokana na utovu
wa nidhamu aliouonyesha kwa kutojumuika kambini mpaka sasa, ikiwa ni wiki moja.
Taarifa za chinichini zinadai chanzo cha
yote, fowadi huyo raia wa Ivory Coast analazimisha kutaka kuondoka kikosini
hapo na kwamba amekuwa akirubuniwa na timu za ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Yanga ndiyo imehusishwa zaidi na kumshawishi
mchezaji huyo bora msimu 2013/14, wakitaka achukue nafasi ya Donald Ngoma
ambaye amezidi kuitoa udenda Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini.
Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba amekiri
Kipre kutofika kambini mpaka sasa na kwamba katika mawasiliano yao hajatoa
sababu za msingi za kuchelewa, hali inayowapa wasiwasi analazimisha kuondoka.
Kawemba ameweka bayana kuwa iwapo kweli kuna
timu inamrubuni, basi ijitokeze kununua lakini akasisitiza thamani yake ni dola
150,000 (Sh milioni 322.1).
“Hajafika mpaka sasa na kila tukiwasiliana
naye anatuambia anakuja leo, kesho na hafiki. Sasa hatujui anawaza nini lakini
ifahamike bado ana mkataba na Azam wa mwaka mmoja na kila kitu juu ya mikataba
yake tunacho sisi.
“Kama kweli anataka kuondoka, thamani yake
ipo wazi. Dola 150,000 na bahati nzuri wachezaji wetu wote kila mmoja thamani
yake ipo kwenye mkataba anaousaini.
“Iwapo kuna timu inamtaka, ije inajua kabisa
thamani yake ni ileile iliyo kwenye mkataba wake,” alisema Kawemba na kusema
kuwa Yanga hawajajitokeza hadharani.
Licha ya hivyo, Kawemba akasisitiza kuondoka
ama kutoondoka kwake hilo wanaliacha mikononi mwa Kocha Zeben Hernandez.
Wakato huohuo, Azam imewaingiza kundini nyota
watatu kutoka Ivory Coast, Benin na Niger ambao wanakuja moja kwa moja kuingia
mikataba kwa kile Kawemba alichobainisha kuwa wameridhishwa na viwango vyao
kwani wamecheza Kombe la Shirikisho Afrika na wapo kwenye timu za taifa.
Akigoma kuwataja majina, Kawemba alisema
lakini Muivory Coast ni straika, Mniger ni kiungo wakati raia wa Benin akimudu
nafasi ya ulinzi.
Post a Comment