SIMBA imeishtukia
kasi ya Yanga katika Ligi Kuu Bara huku yenyewe ikiteleza hivyo klabu hiyo
imepanga kuweka kambi ya muda mfupi nchini Ethiopia kabla ya kuanza kwa
mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Licha ya kuongoza
ligi ikiwa na pointi 35, Simba ilimaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo kwa
kusuasua baada ya kufungwa mechi mbili mfululizo na African Lyon kisha Prisons
na kuzua hofu kwa mashabiki.
Kocha wa Simba,
Joseph Omog raia wa Cameroon ametoa ruhusa ya mapumziko kwa wachezaji wake kwa
muda wa wiki mbili tu kuanzia jana na Novemba 28, mwaka huu wataanza kambi
kujiandaa na mzunguko wa pili.
Mratibu wa Simba,
Abbas Ally ‘Gazza’ alilithibitishia Championi Jumamosi kuwa, wataweka kambi
Ethiopia ambako wamepata mualiko maalum ambapo mbali na mazoezi watacheza mechi
kadhaa za kirafiki.
Mzunguko wa pili
wa ligi kuu utaanza Desemba 17, mwaka huu lakini Omog amesisitiza kukiimarisha kikosi
chake ili kuepuka presha ya Yanga katika kuwania ubingwa.
“Nimetoa likizo
ya wiki mbili na Novemba 28, tutaanza rasmi maandalizi ya raundi ya pili.
Nimefanya hivyo (muda mfupi) kwa kutaka tuwe na maandalizi ya kutosha na
kuhakikisha tunarekebisha makosa tuliyofanya kwenye mechi za mwisho.
“Tageti yangu ya
kwanza nimepanga tupate kambi ya nje ya nchi ambayo itakuwa tulivu na kupata
mechi mbili au tatu za kujipima nguvu,” alisema Omog.
“Ligi ni ngumu na
ninajua Yanga wamefanya vizuri sasa ili tupambane nao vizuri ni lazima tuweka
kambi hiyo kwani naamini tukipata utulivu tutafanya vizuri tukianza ligi.”
Post a Comment