TIMU ya Simba imemalizana kila kitu na kipa wa Medeama, Daniel Agyei na leo Jumatano anatarajiwa kutua nchini kwa ajili ya kusaini mkataba wa kuichezea timu hiyo.
Kipa huyo, atasajiliwa na Simba baada ya kocha mkuu wa timu hiyo Mcameroon, Joseph Omog kutoa mapendekezo hayo kwenye ripoti yake aliyoikabidhi hivi karibuni. Ikumbukwe Ageyi ndiye aliyefungwa na straika wa Yanga, Donald Ngoma kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi ambapo mchezo uliisha kwa sare ya bao 1-1.
Ujio wa kipa huyo, huenda ukamuondoka aliyekuwa kipa namba moja wa timu hiyo Muivory Coast, Vicent Angban kwenye kikosi cha kwanza.
Mkuu wa Kitendo cha Habari na Mawasiliano ya timu hiyo, Haji Manara alisema kipa huyo atatua kwa ajili ya kusaini mkataba wa kuichezeatimu hiyo baada ya kufikia muafaka mzuri.
Manara alisema, kipa huyo mara baada ya kusaini mkataba huo, haraka atajiunga na mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake yaliyoanza jana Jumanne kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam.
"Tumeona maswali yamekuwa mengi, hivyo basi nichukue nafasi hii kutangaza kuwa, kesho (leo) Simba tunashusha kipa mpya kutoka Medeama ambaye ni Agyei raia wa Ghana.
"Kipa huyo, atakuja kusaini mkataba wa kuichezea Simba, hiyo yote ni katika kuifanyia kazi ripoti ya kocha wetu aliyoitoa kwa uongozi katika usajili huu wa dirisha dogo,"alisema Manara.
Kutua kwa kipa huyo, kutafanya idadi ya makipa kuongeza na kuwa wanne ambao ni Manyika Peter Jr, Denis Richard, Angban na Agyei mwenyewe.



Post a Comment

 
Top