TANGU mwaka 1992, ukweli ni kwamba Premier League ilibarikiwa kuwa na wachezaji wenye vipaji vikubwa; baadhi yao ni Steven Gerrard, Paul Scholes, Ryan Giggs, Thierry Henry, Dennis Bergkamp, Cristiano Ronaldo, Luis Suarez na wengine kibao ambao walitengeneza rekodi mbalimbali.
Wakati hao wakizidi kuipaisha ligi hiyo wapo wale ambao walishindwa kabisa kuonyesha uwezo wao hiyo inaweza kuwa hivyo kutokana na kutokopi mfumo au mazingira ya soka la England lakini wengine uwezo wao ulikuwa chini.
Kulikuwa na mabeki ambao walikuwa wanapiga kazi kwelikweli kwa mfano Nemanja Vidic, Rio Ferdinand, Sami Hyypia, Jamie Carragher, John Terry (mpaka sasa anapigana EPL), Kolo Toure, Sol Campbell, hawa wote walikuwa na kauli moja ya mpira uende au wewe ubaki au vinginevyo lakini usipeleke madhara langoni mwao.
Kila kwenye kizuri kibaya hakikosi, wapo walinzi wengine ambao walikuwa wakionekana ni kama hawakuwa na uwezo wa kucheza kwenye ligi hiyo ‘tafu’, yaani mara nyingi walikuwa wakichapia katika kufanya kazi uwanjani, wafuatao ni baadhi yao;

5 Jean-Alain Boumsong (Newcastle United)
Boumsong alijiunga na Newcastle baada ya kiwango chake kukua akiwa katika kikosi cha Auxerre ilichokuwa kikishiriki Ligi Kuu ya Ufaransa. Mfaransa huyu aliwakamua Newcastle pauni milioni nane ambazo zilitumika kumsajilia kwa mkataba wa miaka minne na nusu.
Akiwa katika klabu zake za zamani alionekana kuwa ni mlinzi wa kati aliyekamilika kwani alikuwa na uwezo mkubwa wa kuzuia na pia nguvu alikuwa nazo lakini alishindwa kufanya hayo yote alipokuwa Newcastle. Alikuwa akifanya makosa mengi sana uwanjani kiasi cha mashabiki wa timu hiyo kuanza kuona kama waliuziwa mbuzi kwenye gunia.

#4 Marco Materazzi (Everton)
Nafikiri utakuwa umeshangaa sana kuliona jina hili hapa. Materazzi atakumbukwa kwa namna alivyochezea kichwa cha kifua mbele ya kiungo wa Ufaransa, Zinedine Zidane wakati wa Kombe la Dunia mwaka 2006, ambapo Italia waliibuka machampioni.
Licha ya Materazzi kuharibu mara nyingi akiwa Everton, lakini alifanikiwa kuchukua makombe tofautitofauti kama lile la Serie A akiwa na Inter alichukua mara tano, manne Coppa Italia, manne tena ya Supercopa Italiana, amebeba UEFA Champions League na lile la Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia ‘FIFA Club World Cup’.
Alipokuwa Everton ndiyo alionekana kuwa ‘kimeo’ na kupelekea kukaa msimu mmoja tu kabla ya kuuzwa Perugia iliyokuwa Serie A hapo alivunja rekodi ya kuwa beki aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye ligi, akiweka kambani mabao 12 ndani ya msimu mmoja.


#3 Djimi Traore (Liverpool)        
Traore alijiunga na Liverpool akiwa na miaka 19 hiyo ilikuwa mwaka 1999, alitua kikosini humo akitokea klabu ya nyumbani kwake Laval.
Alidumu Liver kwa miaka saba lakini mara nyingi aliishia kukaa benchi kabla kutimkia kwa majirani zao, Everton.
Akiwa Liver alifanikiwa kucheza kwenye mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya AC Milan ambapo alishindwa kuzuia faulo ya Paul Maldini na kujikuta wakifungwa bao la mapema zaidi, dakika ya tatu.

#2 Roque Junior (Leeds United)
Roque Junior alijiunga na Leeds United mwaka 2003, baada ya msimu huu walijikuta timu yao ikimaliza katika nafsi ya 15 kwenye ligi.
 Mlinzi huyu alionekana kama amekwenda kula mshahara wa bure Leeds kwani uwezo aliokuwa akiuonyesha haukutarajiwa kutokana na kufanya makosa mengi uwanjani.


#1 Pascal Cygan (Arsenal)
Kocha Arsene Wenger alimsaini Pascal Cygan mwaka 2002 baada ya kumuona mlinzi huyo atamfaa ambapo alitokea Lille ya Ligue 1 aliyodumu nayo kwa miaka mingi. Akiwa na matumaini kuwa amesajili jembe litakalomsaidia kikosini mwake jamaa huyo alionekana ‘kumuumiza’ kutokana na kiwango chake kutokuwa na hadhi ya kuchezea Arsenal.
Hata hivyo akiwa Arsenal alifanikiwa kuchukua Kombe la EPL huku akiwemo kwenye kile kikosi cha Invincible.
Licha ya kusubiri kuona kama atabadilika bado hali ilionekana kutokwenda sawa kwani mara nyingi alionekana akishindwa kujipanga uwanjani.
Hata alivyoondoka msimu wa 2005/2006 kwenda Villarreal mashabiki walionekana kufurahia na wala hawakulia kama ambavyo wanafanya kwa wachezaji muhimu wanapoondoka katika timu hiyo.

Post a Comment

 
Top