Yanga wamempa cheo kipya cha Mkurugenzi wa Ufundi Hans van der Pluijm na Mzambia George Lwandamina kupewa nafasi ya ukocha, lakini wenyewe Simba wamejifungia kuimarisha kikosi chao.
Taarifa za uhakika kutoka Simba zinadai kuwa, vigogo hao walikutana kwa siku mbili kujadili ripoti ya Omog, ambapo pamoja na mambo mengine, walikutana na sehemu inayowataka kutafuta majembe manne ya nguvu.
Katika ripoti hiyo ya Omog, inadai kuwa aongezewe straika mmoja, beki mmoja wa kulia na mwingine wa kushoto na pia katika nafasi ya kipa Vincent Angban aongezewe mwenzake mwenye uwezo mkubwa.
Vigogo hao wanajua kuwa, mashabiki wao wanausubiri kwa hamu kubwa ubingwa wa msimu huu, baada ya kukaa kwa misimu minne mfululizo wakishuhudia majirani zao wakitamba na sasa wameanza kunoa makucha yao.
Katika usajili huo, hasa hiyo nafasi ya ushambuliaji, wenyewe walikuwa na mipango kabambe ya kumrejesha Emmanuel Okwi, lakini klabu yake ya SonderjyskE ya nchini Denmark ikaweka ngumu.
Baada ya ugumu huo, taarifa za kuaminika zinadai kuwa wameamua kupeleka nguvu zao nchini Zimbabwe, ambapo mtu wanayemmulika zaidi ni John Chingandu, anayeichezea Zesco.
Taarifa hizo zinasema mipango yote inasukwa na kocha wao wa zamani, Patrick Phiri, huku pia kwa upande wa kipa wakiendelea kuumiza vichwa kuona nani anaweza kufaa kuichezea timu hiyo yenye heshima kubwa ndani na nje ya nchi.
Kuhusu nafasi ya beki wa kulia, licha ya kwamba yupo Janvier Bukungu, Malika Ndeule pamoja na Hamad Juma, taarifa zaidi zinadai kuwa anataka kubakishwa Bukungu peke yake, kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha na wengine wanaweza kutafutiwa timu nyingine.
Kwa upande wa beki wa kushoto, licha ya kwamba yupo Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ,viongozi hao wanataka kumuongezea mwenzake mwenye kasi kubwa ili wawe watatu pamoja na Abdi Banda.
Taarifa kutoka katika kikao hicho zinadai kuwa, vigogo hao wamekubaliana na kocha wao na sasa wanaingia sokoni kwa nguvu zote, huku wakiwatoa wasiwasi mashabiki wao kuwa kilichopo ni kuzidi kuendeleza umoja na mshikamano.
Post a Comment