YANGA haitaki mchezo kabisa, hivyo ndivyo
unavyoweza kusema baada ya kuamua kubadilisha mfumo wake wa kiutendaji ili
kuhakikisha mambo yote ndani ya klabu
hiyo yanakwenda sawa bila tatizo lolote kwa ajili ya maendeleo ya timu.
Mabingwa hao wa Tanzania Bara, juzi Jumamosi
walimshusha Mfaransa, Jerome Dufourg ambaye atakuwa Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo
(CEO).
Dufourg ambaye hapo awali taarifa zake za kutua
Yanga ziliripotiwa na mtandao wa SuperSport, juzi Jumamosi alitua nchini akitokea Ufaransa kwa ajili ya kufanya
mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo uliopo chini ya bilionea Yusuf Manji.
Mfaransa huyo ni jembe kwelikweli. Ni mtaalamu wa
biashara za michezo ambaye ameshatumika sehemu mbalimbali Afrika kwa ajili ya
kuleta maendeleo, hasa katika suala la uwekezaji, masoko, mapato na matumizi.
Ni mbunifu wa njia za kuingiza fedha na anatarajiwa kuifanya Yanga iwe timu
bora Afrika kiuchumi na kiufundi.
Akizungumza na muda mfupi tu baada ya kutua
nchini, Dufourg alisema kuwa amekuja kufanya mazungumzo na Yanga kuhusiana na
kazi hiyo na endapo watafikia makubaliano basi atakuwa mtendaji mkuu wa klabu
hiyo.
“Bado sijamalizana na Yanga, ndiyo kwanza
nimekuja kwa ajili ya mazungumzo , hivyo sitaweza kusema jambo lolote kwa sasa
mpaka hapo tutakapokuwa tumefikia makubaliano.
“Naomba
msinielewe vibaya kwa hilo kwani huo ndiyo utaratibu niliopewa lakini baada ya
mambo kuwa sawa, tutazungumza mengi na tutashirikiana kwa karibu sana ili
kuhakikisha Yanga inapiga hatua zaidi na kuwa timu ya mfano hapa nchini,”
alisema Dofourg.
Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya
Yanga ambazo gazeti hili limezipata, zimedai kuwa mazungumzo yote ya kimkataba
na Dofourg yalishamalizika siku nyingi na kilichokuwa kimebakia ni yeye tu kuja
kusaini mkataba na kuanza kazi.
“Mazungumzo kati ya uongozi na Dofourg
yalishafanyika siku nyingi na walishafikia makubaliano, kilichokuwa bado ni
yeye tu kuja kusaini mkataba, kwa vile amekuja ninachoweza kusema ni kwamba
siku yoyote kuanzia sasa atamalizana na uongozi kisha kuanza kazi, ndiyo maana
amekuja na mabegi mengi jambo ambalo linaashiria kuwa amekuja rasmi kwa ajili
ya kazi,” kilisema chanzo hicho cha habari na kuongeza:
“Endapo mambo yote yatakuwa sawa, kesho (leo)
anaweza kutambulishwa rasmi kwa wanachama na wapenzi na mashabiki wa Yanga kama
CEO wa klabu,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, Katibu Mkuu
wa Yanga, Baraka Deusdedit, hakuwa tayari kuzungumza chochote zaidi ya kudai:
“Sina taarifa zozote kuhusiana na suala hilo.” Aidha Dufourg alifuatilia mchezo
kati ya Prisons na Yanga ulioisha kwa vijana wa Jangwani kushinda bao 1-0 na
kusema: “Nimefuatilia mchezo kati ya Yanga na Prisons, nimekuja na bahati.”
Post a Comment