WAKATI skendo za rushwa zikiendelea kulitikisa soka la Bongo, kipa wa zamani wa Simba, Juma Kaseja, ameibuka na kufunguka kuwa aliwahi kupata skendo ya kutuhumiwa kuhongwa na Yanga ili aruhusu mabao katika pambano moja baina ya timu hizo.

Kaseja, ambaye ni kipa mwenye heshima kubwa nchini, amesema wakati akiichezea Simba mwanzoni mwa miaka ya 2000, viongozi wake walimtuhumu kuwa alihongwa na Yanga baada ya timu hiyo kupokea kichapo cha mabao 2-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mwaka 2003.

Kipa huyo ambaye hivi sasa ana mgogoro na Klabu ya Mbeya City anayoitumikia lakini akiwa hajaichezea mechi yoyote msimu huu, ameweka wazi kuwa hatalisahau tukio hilo.

“Viongozi wangu wa Simba walinituhumu kuwa nilichukua fedha kutoka Yanga ili watufunge, nafikiri ilikuwa ni mwaka 2003 jijini Mwanza ambapo nadhani Yanga walitufunga, hakika siku hiyo niliumia sana.
“Katika mchezo huo Yanga walistahili ushindi kwa sababu sisi tulikuwa tumechoka, tulitoka Afrika Kusini kucheza na Santos ya nchini humo mechi ya Klabu Bingwa Afrika na moja kwa moja tukaenda Mwanza kucheza na Yanga.
“Viongozi wetu bila hata ya huruma yoyote dhidi yetu kuwa tulipoteza mchezo huo kwa sababu ya uchovu, wao wakaamua kuniangushia mimi jumba bovu eti kuwa nimeuza mechi, hakika niliumia sana,” alisema Kaseja katika mahojiano yake maalumu aliyofanya na Gazeti la Championi Jumatatu.

Post a Comment

 
Top