Mbeya City iliisimamisha Yanga baada ya kuifunga mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyopiwa juzi, kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Matokeo hayo yameiwezesha Mbeya City kufikisha pointi 19 baada ya kucheza mechi 14, huku mabao yao yakifungwa na Hassan Mwasapili na Kenny Ally na bao la Yanga likifungwa na Donald Ngoma kwenye mchezo huo.
Akizungumza na BINGWA, Pluijm alisema kikosi chake kilicheza soka bovu kwenye mchezo huo na kuiga mipango ya wapinzani wao ya kupiga mipira mirefu na kusababisha wapoteane uwanjani na kuruhusu bao la mapema lililofungwa na Mwasapili dakika ya sita ya mchezo kipindi cha kwanza.
“Hatukucheza staili yetu tuliyoizoea, tulianza mchezo kwa kucheza taratibu, kuridhika na kuwadharau wapinzani wetu, mwishowe tukaanza kupiga mipira mirefu isiyo na tija kwetu, kiufupi tuliiga mchezo wa wapinzani wetu na kujikuta tunafungwa bao la mapema dakika ya sita.
“Ulikuwa ni mchezo wa kasi ambapo baada ya goli wachezaji walihamaki, badala ya kutulia na kurekebisha makosa yao, mwisho wa siku tukapoteza mchezo, inauma, tunajipanga kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Prisons,” alisema Pluijm.
Katika hatua nyingine, Pluijm alisema ingawa mwamuzi wa mchezo wa juzi, Rajabu Mrope alishindwa kuumudu, lakini kwa upande wake hawezi kumuangushia lawama za moja kwa moja mwamuzi huyo na kusisitiza wachezaji wake walimwangusha.
“Ndiyo mwamuzi hakuwa mzuri na mara nyingi alikuwa akibabaika kutokana na maamuzi yake, lakini nasisitiza hatukucheza kwa staili yetu ya pasi nyingi na kupanga mipango ya ushindi, walidharau mchezo,” aliongeza Pluijm.
Pluijm alisema alimwanzisha kiungo Mbuyu Twite kucheza eneo la chini kwenye mchezo huo, lengo likiwa kuziba eneo la kati na kujilinda, hususan wanapokutana na timu zinazokamia au zenye viungo wazuri.
Hata hivyo, mbinu hizo zilishindwa kufua dafu mbele ya Kocha wa Mbeya City, Kina Phiri, ambaye aligundua mapema na alichokifanya ni kitu kidogo tu, kujaza viungo wengi eneo la kati na kumlazimisha Mbuyu Twite kucheza mstari mmoja na walinzi wa kati na kukata kombinesheni yake na Haruna Niyonzima, hali iliyowafanya Yanga kuwaongezea eneo la kupanga mashambulizi yao mbele ya City.
Post a Comment