IKIWA tayari imeshikilia rekodi mbili kwa mpigo msimu huu, ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Stand United juzi Jumatano, uliifanya Simba kuandika rekodi nyingine msimu huu, ikiwa ni timu ya kwanza kuchukua ushindi kwenye Uwanja wa Kambarage dhidi ya Stand.

Kwanza, kikosi hicho chini ya Joseph Omog ndicho kinashikilia rekodi ya kutopoteza mchezo wowote katika mechi 12, ikiwa ni mara ya kwanza tangu msimu wa 2009/2010 ilipotwaa ubingwa bila kupoteza mchezo wowote na rekodi nyingine ni ya kucheza mechi nyingi bila kuruhusu bao ‘clean sheet’. Katika mechi 13, imeruhusu bao kwenye mechi tatu tu; dhidi ya Ndanda, Ruvu Shooting na Yanga.

Bao pekee lililofungwa na kinara wa mabao, Shiza Kichuya dakika ya 33, liliiwezesha Simba kung’ang’ania kileleni kwa kufikisha pointi 35, kichapo kilichoifanya Stand United ipoteze mchezo wa kwanza nyumbani tangu kuanza kwa msimu huu, ikiwa na kumbukumbu ya kuzichapa Azam na Yanga uwanjani hapo.


Takwimu zinaonyesha Stand imecheza mechi nane katika Uwanja wa Kambarage ambapo imeshinda mechi nne; dhidi ya Toto, Yanga na Azam (zote 1-0) na dhidi ya JKT mabao 2-1). Ilitoa suluhu na Mbao kisha sare ya 2-2 na Mwadui kisha 1-1 na Lyon.

Akizungumzia rekodi, Mcameroon Omog alisema siri ya yote ni umoja, nidhamu ya kazi na juhudi binafsi za wachezaji katika kufikia malengo.

“Nafikiri ni matokeo ya kujituma kwa wachezaji na kukubali kuwa tayari kupigana mpaka dakika ya mwisho ya mchezo kwa kila mechi tunayocheza. Siyo kwamba kuna jambo geni nililowapa wachezaji, zaidi ya wao kujitambua, kukubali kupigana kufikia malengo yetu ya safari hii (ubingwa),” alisema Omog.

Simba itakwaana na Lyon, keshokutwa Jumapili itakuwa mgeni wa African Lyon kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar ambayo juzi Jumatano ilichezea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting.


Post a Comment

 
Top