YANGA ilipata kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa
Mbeya City katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa, lakini
nyuma ya pazia kuna mambo kadhaa ambayo yalifanyika na kikubwa kinachotajwa ni hujuma
ili Yanga ipoteze mchezo huo.
Kufungwa kwa Yanga katika mchezo huo ni pigo
kubwa kwao kwa kuwa sasa wameachwa kwa pointi nane dhidi ya Simba ambao ndiyo
wanaoongoza ligi hiyo wakati Yanga wakishika nafasi ya pili wakiwa na pointi
27.
Akizungumza na gazeti hili kabla ya mchezo huo
uliochezwa juzi Jumatano, kiongozi mmoja wa Yanga ambaye yupo Mbeya, alianza
kusema kuwa kulikuwa na kampeni kubwa iliyofanyika kuhakikisha Yanga inafungwa
na hiyo inafanywa kuanzia ngazi za juu za uongozi wa mkoa.
Yanga
yazuiwa kufanya mazoezi
Muda mfupi kabla ya mchezo huo, kigogo huyo
alikutana na Championi Ijumaa na kufunguka:
“Kuna hujuma ya kiwango cha juu inafanyika ili
tufungwe, mimi nilizipata hizo taarifa hata kabla ya timu (Yanga) kufika hapa
Mbeya, niliambiwa hadi (anataja jina) anahusika kwenye kampeni hiyo.
“Kuna figisu nyingi zimefanyika kabla ya
mchezo, jana (Jumanne) tulitakiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Sokoine, asubuhi,
tulipofika hapa tukawakuta makomandoo wa Mbeya City, wakagoma kutupisha wakati
utaratibu unasema sisi pia tunatakiwa kufanya mazoezi uwanjani hapo siku moja
kabla ya mchezo.
“Tulichofanya tukaanza kuwasiliana na mamlaka
husika watusaidie, lakini huko nako chenga zikawa nyingi, baadaye tukawasiliane
na mamlaka za juu kabisa za mkoa kiusalama kuja kutusaidia, napo tulianza
kupigwa chengachenga awali.
“Baadaye kidogo jeshi la polisi likafika
uwanjani hapo na kuwaondoa makomandoo hao, ndipo ukaruhusiwa kufanya mazoezi.”
Jioni hali
ikawa tete
“Baadaye jioni Yanga ilikuwa na ratiba ya
kufanya mazoezi tena uwanjani hapo, lakini hilo halikuwezekana kwa kuwa makomandoo
wa Mbeya City walikuwepo na kulitokea vurugu nyingi kati yao na sisi, mwisho
timu haikufanikiwa kufanya mazoezi kabisa,” anasema kiongozi huyo.
Vurugu
usiku, kulinda uwanja
Taarifa zinaeleza usiku wa kuamkia mchezo huo,
kulitokea vurugu pia baina ya wasimamizi wa Yanga na Mbeya City ambao wote
walikuwa wakitaka kulinda uwanja huo.
“Kulikuwa na pande tatu zinazolinda, Yanga,
Mbeya City na Suma JKT ambao ndiyo walinzi wa siku zote wa uwanja huo,” alisema
shuhuda wa tukio hilo.
Alipotafutwa Meneja wa Uwanja wa Sokoine,
Vedastus Mwaluka, alisema: “Ni kweli kulikuwa na vurugu usiku, wale watu wa
Yanga na Mbeya City walikuwa wakifanyiana vurugu sana kuanzia asubuhi
(Jumanne).
“Kwanza ile ya asubuhi Yanga ndiyo walitakiwa
kufanya mazoezi na walichokifanya Mbeya City kuwafanyia wenzao vurugu kwa kweli
sikukipenda. Yanga walipiga simu polisi ambao walifika na kutatua mgogoro
uliokuwepo.
“Jioni pia kulitokea mvurugano baina ya pande
hizo mbili, usiku napo hali ikawa hivyohivyo, ubabe wao uliwazidi nguvu wale walinzi
wa Suma JKT na hivyo nikalazimika kupiga simu polisi, walifika na kuwatoa wote
hali ikatulia, mpaka naondoka uwanjani saa nne kasoro usiku, niliacha pametulia
na kuwataka Suma JKT kama kukitokea chochote wanijulishe.”
Post a Comment