SIKU chache baada ya Simba SC kumaliza mapitio ya ripoti ya mzunguko wa kwanza kama ilivyowasilishwa na kocha Joseph Omog ambaye alibainisha kuboreshewa kikosi, panga la kwanza limemuangukia beki Malika Ndeule ambaye kwa taarifa rasmi hana chake tena.

Kabla ya kuondoka kwenda kwao Cameroon, Omog aliliambia Championi kuwa ripoti yake alipendekeza kuongezewa sura mpya chache kwani bado anaamini mpaka raundi ya kwanza Simba ndiyo ilikuwa na kikosi bora lakini akaomba baadhi ya wachezaji si zaidi ya watatu kuachwa kutokana na kutokuwa na msaada.

Chanzo cha ndani kimeliambia gazeti hili kuwa Malika amekuwa mhanga wa kwanza kwenye panga la Mcameroon huyo lakini pia wakiwa kwenye msako wa kutafuta kipa mwenye uzoefu ambaye atampa changamoto Muivory Coast, Vincent Angban kama kocha alivyopendekeza.
Katibu wa Simba, Patrick Kahemele amekiri kuwa kwenye mchakato wa kumpa kipa huyo lakini akasisitiza kuwa ni lazima awe mzawa.
“Kocha aliomba apatikane kipa mwenye uzoefu na awe mzawa, tofauti na watu wanavyosema kuwa ni wa kimataifa. Mchakato huo upo, unashughulikiwa na kamati ya usajili, wao ndiyo wanahusika na kila jambo la usajili,” alisema Kahemele aliyekanusha taarifa za Malika kutemwa.
Alipotafutwa Malika mwenyewe baada ya kuulizwa swali hilo akasema: “Naomba uniache kwa sasa maana niko msibani, nikitoka nitakupigia.”

Post a Comment

 
Top