SIMBA ipo katika mkakati wa kumsajili
kipa atakayempa changamoto Vincent Angban, hesabu zikaangukia kwa Aishi Manula
wa Azam FC lakini sasa mambo yamekuwa magumu kwao.
Manula bado ana mkataba na Azam hivyo
Simba ilitaka kumsajili kwa mkopo lakini kipa huyo akawaambia kama wanamtaka
wavunje mkataba wake ili acheze akiwa mali yao jumla.
Bosi mmoja wa Kamati ya Usajili ya
Simba, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, sharti hilo la Manula limewarudisha
nyuma katika harakati zao za kumsajili kwani ni ngumu kwao kuvunja mkataba
wake.
“Ripoti ya kocha inataka tumsajili
kipa mmoja mzoefu katika Ligi Kuu Bara, tukaona Manula anatufaa lakini yeye
bado ana mkataba na Azam tukamuomba kwa mkopo ili aje kumpa changamoto Angban.
“Amekataa kuja kwa mkopo badala yake
anataka tuvunje mkataba wake jambo ambalo ni gumu kwetu kulifanya hivi sasa, Azam
walitaka kukubali lakini mchezaji mwenyewe amegoma,” alisema bosi huyo.
Kutokana na hali hiyo, Simba
inaendelea na mchakato wa kutafuta kipa mwingine atakayeweza kuleta changamoto
kwa Angban huku kikosini ikiwa na makipa wengine Peter Manyika Jr na Dennis
Richard.
Akizungumzia mchakato huo wa Simba
uliokwama, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Azam, Idrissa Nassor alisema: “Manula siyo
embe useme utaligawa kwa mtu yeyote yule, huyu ni mchezaji wetu tunayemtegemea
na sasa hatuna mpango wa kumuuza au kumtoa kwa mkopo badala yake tunataka kuongeza
kipa mwingine.”
Post a Comment