MWANACHAMA na mfadhili wa zamani wa klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, ameingilia kati suala la usajili wa beki wa kushoto wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, kwa kutoa fedha za kumuongezea mkataba mpya. Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo na taarifa kuwa saini ya mchezaji huyo ipo kwenye rada za mahasimu wao Yanga ambao wameonyesha nia ya kutaka kumsajili kwenye dirisha dogo.
Habari za uhakika zilizolifikia BINGWA jana kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, zinasema kuwa Tshabalala kwa sasa amebakisha miezi sita kwenye mkataba wake na Simba, ambapo kisheria mchezaji akibakisha miezi hiyo anaruhusiwa kuanza mazungumzo na klabu nyingine yenye nia ya kumsajili.
Kwa kuhofia hilo, Simba imeamua kuanza kuwatia ‘vitanzi’ wachezaji wake ambao mikataba yao ipo mwishoni akiwemo Tshabalala na Abdi Banda, ambao tayari wameanza nao mazungumzo ya mikataba mipya.
MO ambaye alikuwa kwenye mchakato wa kununua hisa 51 za klabu hiyo katika mchakato wa mabadiliko ambao ulisimishwa na Serikali, ameamua kunusuru jahazi hilo kwa kutoa pesa za kuwaongezea mikataba wachezaji hao na kulipa mishahara ya wachezaji wengine waliokuwa wanadai mishahara yao.
“MO ameamua kutoa fedha za kuwaongezea mikataba mipya wachezaji ambao mikataba yao ipo mwishoni, akiwamo na Tshabalala na wengine lakini pia tayari wachezaji wote waliokuwa wanadai mishahara yao wameshalipwa, hivyo kila kitu kipo sawa,” alisema mtoa habari huyo.
BINGWA lilizungumza na Mkuu wa kitengo cha timu hiyo, Haji Manara, ambaye alisema kuwa suala la mkataba ni baina ya timu na mchezaji, hivyo hawezi kuweka wazi suala hilo iwapo kama wameanza mazungumzo ya mkataba mpya au la.
“Hilo ni suala la siri baina ya klabu ya mchezaji husika, hivyo hatuwezi kuweka wazi,” alisema Manara.
Katika hatua nyingine, klabu ya Simba inadaiwa kuwa imekamilisha usajili wa straika Mganda, Emanuel Okwi ambaye anadaiwa kurudi nchini kuungana na klabu yake hiyo ya zamani kwa dau la Dola 100,000 (Sh milioni 220).
Lakini licha ya kuenea kwa taarifa hizo, klabu hiyo imekanusha kuhusu ujio wa Okwi na kuweka wazi kuwa timu hiyo bado haijaongeza mchezaji yeyote mpya kwenye kikosi chake.
Habari hii imeandaliwa na SALMA MPELI NA MARY PETER (TSJ)

Post a Comment

 
Top