VINARA wa Ligi Kuu Bara, Simba, wamerejea Dar es Salaam na kwenda kujichimbia Hoteli ya Dege Beach, inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Bweni), nje kidogo ya jiji kujiandaa na mechi dhidi ya African Lyon, itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru.
Kikosi hicho kilitarajia kurejea jana jioni kwa ndege kikitokea Shinyanga, ambako walikuwa na mechi mbili za ligi hiyo kati ya Mwadui FC na Stand United.
Akizungumza na BINGWA, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Haji Manara, alisema timu hiyo imerejea jana jioni na moja kwa moja imekwenda kambini.
“Timu imerudi Dar na ndege na moja kwa moja imekwenda Dege Beach ambapo inajiandaa na mchezo unaofuata dhidi ya African Lyon,” alisema.
Alisema ushindi wao walioupata mkoani Shinyanga ambao umesababisha kumuacha mpinzani wake, Yanga kwa pointi nane kamwe haumpi kiburi.
“Tunaongoza kwa pointi nane, lakini si kwamba unatupa kiburi ndiyo sababu ya kuingia kambini moja kwa moja kwa ajili ya kujiandaa na Lyon,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu Yanga, Manara alisema Simba msimu huu inafanya yake bila ya kuangalia ya timu pinzani, huku akimaliza kwa kuwapa kijembe mahasimu wake hao wa jadi kuwa mwaka huu watafungwa sana.
Simba ndio wanaongoza ligi kwa sasa kwa kuwa na pointi 35, huku wakiwa wamecheza michezo sawa na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wenye pointi 27 mpaka sasa.

Post a Comment

 
Top