KOCHA wa Simba, Joseph Omog mjanja
sana kwani amewaambia viongozi wa Simba ana nafasi tatu za wachezaji ambao
anataka wamuongezee nguvu kikosini.
Mmoja wa mabosi wa Kamati ya Utendaji
ya Simba ambayo ndiyo ya kwanza kuona ripoti ya kocha, amesema kuwa, anataka
wamsajilie kipa, beki na straika mmoja.
Katika ripoti yake, Omog ametoa sifa
tu za wachezaji anaowataka huku akiacha zoezi la kuwasajili kwa viongozi lakini
akasisitiza haitaji straika kutoka nje ya nchi kwani atapata presha kama ilivyo
kwa waliopo.
Simba ina mastraika Laudit Mavugo raia
wa Burundi na Fredrick Blagnon wa Ivory Coast ambao bado hawajaonyesha uwezo
mkubwa katika Ligi Kuu Bara katika mechi 15 za Simba.
Kabla ya kuiona ripoti ya Omog, baadhi
ya viongozi wa Simba ambao wameona Mavugo na Blagnon walivyochemsha, wakaanza
mipango ya kumrejesha kikosini Emmanuel Okwi kutoka SønderjyskE ya Denmark.
“Kutokana na ripoti ya Omog, sasa
hatuna tena mpango wa kumsajili Okwi kwani itakuwa kinyume na matakwa ya kocha
hivyo tunaendelea na mambo mengine kwa kufuata anachotaka yeye (Omog).
“Tulidhani Okwi akija atafanya vizuri
moja kwa moja kwani anaijua ligi yetu, lakini kocha ameshikilia msimamo wake wa
kutaka straika kutoka ndani ya nchi, hatuna jinsi tunafuata kile alichosema,”
alisema bosi huyo.
Licha ya viongozi wake kutokuwa tayari
kuweka wazi kuhusu usajili wa straika mzawa, gazeti hili linafahamu Simba
inamfukuzia Victor Hangaya wa Prisons ili iweze kumsajili.
Post a Comment