KOCHA Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, kesho ataanza rasmi kibarua chake ndani ya kikosi hicho, lakini kabla ya hapo amekutana na mtangulizi wake, Hans van der Pluijm kwa siku tatu, sawa na saa 72, kuweka mambo sawa.
Wachezaji wa Yanga ambao walikuwa mapumziko baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, wanatakiwa kujikusanya wote kufikia leo Jumapili na kesho bila kupoteza muda wawepo mazoezini kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili na michuano ya kimataifa, ambapo mara hii watakuwa na kocha mpya ambaye ni Lwandamina.
Lwandamina, ambaye awali alikuwa amewekwa mafichoni, alitambulishwa rasmi Ijumaa ya wiki hii na baada ya utambulisho huo Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga, akasema kocha wao huyo mpya anakwenda kukaa na Pluijm ili kuanza mikakati yao.
Wawili hao watashirikiana kwa kila jambo, kwani Pluijm amepewa kazi ya ukurugenzi wa ufundi ndani ya klabu hiyo na sasa lazima wapange mikakati kwa pamoja, lengo likiwa kuiona Yanga ikiwika kitaifa na kimataifa watakaposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Akizungumza juzi Ijumaa katika utambulisho wake uliofanyika makao makuu ya klabu hiyo, mitaa ya Twiga na Jangwani, Sanga alisema baada ya kumaliza kumtambulisha mgeni wao huyo, kilichobakia ni kwenda kukaa na Pluijm waanze mambo yao kabla ya mazoezi kesho.
“Jamani tumalizeni haraka, kwani wanakwenda kukutana (Pluijm na Lwandamina) ili kuanza mikakati yao ya kuijenga Yanga, kwani timu inakabiliwa na mambo mengi na yote yanatakiwa yafanyike kwa ufanisi mzuri,” alisema Sanga na kuwafanya mashabiki waliokuwepo kwenye utambulisho huo nyuso zao kuonyesha matumaini.
Kauli hiyo inamaanisha kuwa, Pluijm na Lwandamina walianza mikakati yao hiyo Ijumaa, jana wakawasiliana, na leo siku ya tatu wanamalizia vikao vyao kabla ya kesho kuanza kibarua kila mmoja akiwa na majukumu yake mapya.
Katika mikakati yake, Lwandamina alisema anahusudu namna Barcelona ya nchini Hispania inavyocheza, hiyo ikimaanisha kuwa anakuja na soka la kisasa la pasi fupifupi na za uhakika, huku wakitakiwa kumiliki mpira kwa muda wote na pale wanaponyang’anywa kila mmoja anakuwa na jukumu la kuhakikisha wanawapora wapinzani wao haraka iwezekanavyo.
Kuhusu Yanga wanavyoonewa na timu za Kiarabu, Lwandamina amesema unyonge huo sasa basi na kwamba ushirikiano wake na Pluijm, ambaye ni mkurugenzi wa ufundi, utawafanya wana Yanga kufurahi muda wote, isipokuwa kubwa aliloliomba ni ushirikiano.
Yanga mwakani wanaiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na jambo ambalo Lwandamina anatamani liwe ni kuiona timu yake hiyo mpya ikifanya maajabu ambapo amesema hilo linawezekana kutokana na uzoefu wake na pia uzoefu alionao Pluijm.
Kuhusu kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mashabiki wa Yanga wanatakiwa kuondoka shaka kabisa, kwani licha ya Simba kuongoza kwa sasa, lakini Lwandamina amesema kila kitu kitakwenda vizuri.
Post a Comment