STRAIKA wa Kimataifa wa Simba, Mrundi Laudit Mavugo, anajua kuwa hakufanya vizuri kama ilivyotarajiwa katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na sasa ametumia mapumziko yake kujifua na timu yake ya zamani ya Vital’O kwa ajili ya kuongeza makali.

Mavugo aliianza ligi vizuri, akifunga bao kwenye ushindi wa mabao 3-1 Simba walioupata dhidi ya Ndanda FC, katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu, lakini kadri siku zilivyokuwa zikienda ndivyo kiwango chake kilivyokuwa kikiporomoka.

Mavugo amesema, anatumia vizuri likizo yake kuhakikisha anaendelea kujiweka fiti kwa ajili ya kufanya vizuri katika timu yake kwenye mechi za mzunguko wa pili wa Ligi hiyo.

“Najua kuwa kuna kazi kubwa ya kufanya, ndiyo maana nimeamua kujifua kikamilifu kuhakikisha najiweka fiti, naamini mambo yatakuwa mazuri na timu yetu itaendelea kukaa kileleni,” alisema.

Akizungumzia harakati za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, alisema licha ya kwamba kila timu imejipanga, lakini Simba wapo vizuri zaidi na kilichobakia ni ushirikiano kwa kila upande.

Post a Comment

 
Top