KOCHA
wa Yanga, Hans van Der Pluijm amesema atahakikisha timu yake inaifunga Prisons,
kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa lakini wachezaji wa timu
hiyo wameiambia Simba kamwe isijidanganye kuhusu kutwaa wa Ligi Kuu Bara
ubingwa msimu huu.
Pluijm
baada ya kupoteza mechi dhidi ya Mbeya City, Jumatano wiki hii kwa kufungwa
mabao 2-1, amesema atahakikisha wanapata pointi tatu dhidi ya Prisons na
kupunguza tofauti ya pointi kati yao na Simba.
Simba
ipo kileleni mwa ligi kuu ikiwa na pointi 35 katika mechi 13 kama ilizocheza
Yanga yenye pointi 22 ikiwa nafasi ya pili.
“Mambo
mengi yalitokea tukapoteza dhidi ya Mbeya City, lakini hiyo haiwezi kuwa maana
ya kupoteza mechi zote za Mbeya, tuna mechi na Prisons naamini tutafanya vizuri
baada ya maandalizi ya uhakika.
“Tumebadilika
kidogo hasa katika mbinu ili tuweze kupata pointi tatu ambazo zitapungua pointi
kati yetu na timu inayoongoza, naamini itakuwa hivyo,” alisema Pluijm.
Naye
Kocha wa Prisons, Meja Mstaafu Abdul Mingange alisema: “Watu wasione Yanga
sababu imefungwa na Mbeya City basi na sisi ni lazima tuifunge, soka halipo
hivyo lakini hatutakubali kufungwa na Yanga.
“Yanga
ni timu kubwa yenye uzoefu na inayojua kupambana, sasa mashabiki wategemee soka
la ushindi uwanjani ila wasidhani kama kila kitu ni kirahisi.”
Straika
Amissi Tambwe na nahodha wa Yanga, Haruna Niyonzima, kwa pamoja wamesema
kufungwa na Mbeya City hakujawakatisha tamaa ya kutetea ubingwa wao na kamwe
Simba wasijidanganye.
“Simba
wasijidanganye kuhusu ubingwa eti kwa sababu wanaongoza, bado kuna mechi nyingi
mno ambazo zinaweza kuwaweka chini na sisi tukaibuka,” alisema Tambwe.
Naye
Niyonzima alisema: “Kupoteza mechi mbili inauma sana, lakini hiyo si sababu ya
kupoteza ubingwa na Simba japokuwa wanaongoza ligi wasidhani sisi tumelala,
hapana kilichotokea kwetu ni bahati mbaya tu.”
Post a Comment