KAMA unadhani kocha mkuu wa Simba, Joseph Omog, amebweteka
na pointi 35 walizonazo kileleni, unakosea kwani Mcameroon huyo anawaza kupata
pointi nyingine leo dhidi ya African Lyon.
Wekundu hao wa Msimbazi watakuwa Uwanja wa Uhuru kucheza na
African Lyon ambapo Omog ametamba kuwa kilichopo kichwani mwake ni kuhakikisha
wanaondoka na pointi tatu muhimu.
“Kwetu kila mchezo ni fainali, tunataka kumaliza mzunguko wa
kwanza bila kupoteza na hilo linaweza kutimia kutokana na maandalizi mazuri
tuliyoyafanya,” alisema.
Simba itashuka dimbani ikiwa na matumaini makubwa ya
kumtumia mshambuliaji wake, Fredrick Blagnon ambaye hakuwepo katika michezo
miwili iliyopita kutokana na kuwa majeruhi baada ya kuumia katika mchezo dhidi
ya Toto Africans.
Blagnon amerejea kikosini ambapo juzi na jana alijiunga na
wenzake katika mazoezi yaliyofanyika Uwanja wa Boko Veterani na kuna asilimia
kubwa ya kutumika katika mchezo wa leo.
Simba wapo kileleni wakiwa na pointi 35 wakiwa hawajapoteza
mchezo wowote huku Yanga wakifuata katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 27 na
sasa Wekundu hao wa Msimbazi wanataka kuwaacha mbali wapinzani wao hao.
Katika mchezo huo Simba itaendelea kuwaamini washambuliaji
wake wakiongozwa na Shiza Kichuya mwenye mabao tisa kileleni, Mohamed Ibrahim,
Ibrahim Ajib pamoja na Laudit Mavugo.
Wakati Simba mambo yakiwa mazuri, kwa upande wao African
Lyon huenda ikakosa baadhi ya wachezaji wao tegemeo akiwemo Hood Mayanja na
Tito Okelo pamoja na William Otong’o.
Hata hivyo, kocha mkuu wa kikosi hicho, Fernando Jose
Bernado, alisema kikosi chake kipo vizuri na atahakikisha wanaondoka na pointi
zote tatu.
Post a Comment