KWA sasa anatajwa kuwa miongoni mwa mabeki bora wa kushoto nchini Tanzania. Uwezo wake ndani ya kikosi cha Simba ndio uliomfanya Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa, amuite kikosini mwake.
Uwezo wa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ dimbani unatajwa kuzikuna baadhi ya klabu za Ligi Kuu, ikiwemo Yanga, ambapo walianza kumpigia mahesabu makali namna ya kuipata saini yake msimu ujao wa ligi hiyo.
Tshabalala ni miongoni mwa nyota ambao ni zao la kikosi cha vijana cha Azam FC, aliyepandishwa timu ya wakubwa kabla ya kutolewa kwa mkopo Kagera Sugar na baadaye kwenda Simba.
DIMBA limefanya mazungumzo ya kina na beki huyo anayetajwa kuwa ni hazina kubwa ya Taifa kwa sasa iwapo atatunza kiwango chake.
DIMBA: Unaingaliaje Simba ya msimu huu na nini maoni yako kwa siku zijazo kwa kikosi hiki?
Tshabalala: Ni timu nzuri, nina imani kubwa ya kufanya vizuri kwa msimu huu, kulingana na usajili uliofanywa.
DIMBA: Katika michezo 15 mliyocheza katika mzunguko wa kwanza, straika gani unayemhofia?
Tshabalala: Nasema kutoka moyoni straika wa kimataifa wa Yanga, Donald Ngoma, raia wa Zimbabwe ndiye aliyenisumbua sana, kwani jamaa ni mashine hatari nje na ndani ya eneo la 18. Ukifanya kosa lolote mbele ya Ngoma lazima atakuadhibu.
DIMBA: Jina la Tshabalala ulilipataje?
 Tshabalala: Nampenda Lawrence Siphiwe Tshabalala, raia wa Afrika Kusini ambaye anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji katika kikosi cha Kaizer Chiefs. Nakumbuka wakati nikicheza kwenye kikosi cha Boom Boom, nilikuwa navaa jezi ya Afrika Kusini iliyoandokwa Tshabalala, hivyo watu wakawa wananiita jina hilo.

DIMBA: Ulipataje nafasi Kagera Sugar?
Tshabalala: Henry Mzozo alifanya mazungumzo na Kocha Kibadeni (Abdallah) ambaye alinipa nafasi ya majaribio. Mwisho wakaniambia twende Bukoba na baadaye wakanisajili. Lakini sikuwa na bahati na Kagera, hasa siku za mwanzoni.
DIMBA: Soka ni juhudi, bahati kivipi?
Tshabalala: Mwanzoni nilipofika tu nikaitwa timu ya taifa ‘Under 20’, baada ya kurejea Bukoba nikaumia na kukaa nje nusu msimu.
DIMBA: Nini kilikufanya ukataka kwenda Ulaya mapema hata kabla ya kujiunga na Simba?
Tshabalala: Baba yangu mdogo anayeishi Uholanzi akanishauri kusajili timu itakayokubali mkataba wa mwaka mmoja tu, ili baadaye niende kufanya majaribio Ulaya, nikakubali.
DIMBA: Yanga wamekuja kuhusu kuhitaji saini yako, je, kuna ukweli juu ya hili?
Tshabalala: Hayo ni maneno ambayo yapo, kwa upande wangu hakuna kiongozi wa Yanga aliyenifuata kwa ajili ya kuhitaji huduma yangu.
DIMBA: Nini unakiona ni changamoto, hasa unapokutana na washambuliaji watukutu?
 Tshabalala: Wapo baadhi ya wachezaji wanakuwa si waungwana, kwa maana wanapokuwa uwanjani wanatumia mbinu chafu ili kukutoa mchezoni, ikiwemo kunitukana lakini nimekuwa nikivumilia.
DIMBA: Wewe ni  shabiki wa timu gani Ulaya, pia ungependa kucheza wapi nje ya Tanzania?
Tshabalala: Manchester United ndiyo chama langu. Nikitoka nje naweza kuanza Afrika Kusini na kama Ulaya, sehemu yoyote ambayo nitapata timu bora.
DIMBA: Unadhani kubadilisha makocha mara kwa mara ndiyo sababu ya kuyumba kwa timu ya Simba kiasi cha kuwaathiri wachezaji kwa misimu iliyopita?
Tshabalala: Hilo la kubadili makocha lina ukweli kwa upande mmoja, kwa sababu wakati mwingine timu inapotea baada ya kocha mgeni kuja na mfumo au falsafa tofauti.
DIMBA: Licha ya soka, je, kuna mchezo mwingine unacheza?
Tshabalala: Hapana, sina mwingine zaidi ya soka, nahisi hiyo ilikuwa ndoto yangu tangu nilipokuwa shule na sasa nimeitimiza.
DIMBA: Umesema soka lilikuwa ndani ya moyo, mfano soka lingekukataa unadhani ungefanya kazi gani?
Tshabalala: Ni kweli kuna mipango mingine huwa inakataa, lakini kwangu ningekuwa mfanyabiashara.
DIMBA: Unaishi wapi na umeoa au una mtoto?
Tshabalala: Naishi Magomeni, sijabahatika kupata vyote, nikimaanisha mtoto wala mke.
DIMBA: Ukiwa nyumbani ni shughuli gani ambazo unajishughulisha nazo?
Tshabalala: Napenda kuangalia filamu na kujishughulisha na kazi za nyumbani.
MAKALA HII IMETOKA KWENYE GAZETI LA DIMBA LILILOPO MTAANI LEO

Post a Comment

 
Top