Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu Wanawake ‘Twiga Stars’ jana
Novemba 10, 2016 ilipoteza kwa taabu mchezo wake wa kwanza wa kirafiki wa
kimataifa dhidi ya wenyeji Cameroon ambayo ilipata mtihani mzito kwa Watanzania
kwa dakika zote kabla ya kuibuka kwa ushindi wa mabao 2-0.
Cameroon ambayo ilijipanga kushinda mabao mengi, ilitolewa
jasho na hivyo kuomba mchezo mwingine ambao sasa utafanyika Jumapili Novemba
13, mwaka huu jijini Yaounde na Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Sebastian Nkoma
amesema: “Nimeona upungufu katika mchezo wa jana, nafanyia kazi.”
Bao la kwanza katika mchezo wa jana lilifungwa na
Mshambuliaji Ngoya Ajara wa Klabu ya Sundsvalls ya Sweden ambaye pia ndiye
Mchezaji Bora wa mwaka 2016 nchini Cameroon wakati bao la pili lilifungwa na
Kiungo wa Klabu ya Aurillac ya Ufaransa Ngono Mani Michelle katika dakika ya
71.
Twiga Stars wao wamealikwa na Waandaaji wa fainali za Kombe
la Mataifa ya Afrika kwa wanawake 2016 – Cameroon ambao wameamua kuipa heshima
Tanzania na kuona kuwa timu hiyo ina ubora wa na kwamba inafaa kuipimana ubavu
kabla ya kuanza kwa fainali hizo Novemba 19, mwaka huu.
Twiga Stars ambayo sehemu kubwa ya kikosi hicho kinaundwa na
wachezaji wa timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania Bara yaani Kilimanjaro
Queens ina rekodi nzuri ya kuwa kinara wa viwango vya ubora kwa nchi za Afrika
Mashariki na kati lakini zaidi ni mabingwa wapya wa ukanda huo – ubingwa
uliopatikana Septemba, mwaka huu huko Uganda.
Rekodi hizo zimesukuma Shirikisho la Mpira wa Miguu la
Cameroon (FECAFOOT) – nyumbani kwa Rais wa CAF, Issa Hayatou kuikubali Twiga
Stars na hivyo kuomba kucheza nayo mwishoni mwa wiki hii. Tayari Twiga Stars
imeanza maandalizi ya kutosha chini ya Makocha Sebastian Nkoma na Wasaidizi
wake Edna Lema na El Uterry Mohrery.
Kikosi cha Twiga Stars wamo makipa, Fatma Omari na Najiat
Abbas; mabeki ni Wema Richard, Sophia Mwasikili, Anastasia Katunzi, Maimuna
Hamisi, Fatuma Issa, Happiness Mwaipaja na Mary Masatu wakati viungo ni Donisia
Minja, Stumai Abdallah, Amina Ally, Anna Mwaisura na Fadila Kigarawa ilhali
washambuliaji ni Fatuma Swalehe, Asha Rashid na Mwanahamisi Omari.
Post a Comment