KOCHA Msaidizi wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja ametamka kuwa hakuna chochote kilichowasababishia wapoteze mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara zaidi ya kuzidiwa mbinu na wapinzani wao.

Timu hiyo, jana ilipoteza mchezo wa pili walipovaana na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya kwa kufungwa mabao 2-1 wakitoka kufungwa na African Lyon bao 1-0 mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.

Mayanja amesema kwa kushirikiana na bosi wake Mcameroon, Joseph Omog walifanya kila liwezekano ili kupata ushindi kwenye mechi na Lyon na Prisons, lakini bahati haikuwa ya kwao.

Mayanja alisema, wapinzani wao wote walitumia mbinu za kucheza kwa kujilinda zaidi golini kwao kwa kujaza mabeki nyuma watatu kwenye mechi hizo zote na kusababisha kuzikosa pointi sita.

Aliongeza kuwa, katika mechi hizo zote walijitahidi kubadili mifumo mbalimbali baada ya kuwaona wapinzani wao wakicheza soka la kujilinda zaidi, lakini walishindwa kuvuna pointi na kujikuta wakifungwa.


“Katika mechi hizo zote ambazo Simba tumefungwa, sidhani kama wapinzani wetu walituzidi kimchezo, wao walichobahatika kupata bahati kwa kutengeneza nafasi za mabao na kuzitumia vizuri, ninaamini na sisi tungezitumia hizo nafasi tulizozipata, basi matokeo yasingemalizika kama hayo tuliyoyapata.

“Mechi ya African Lyon wao walicheza kwa kujilinda kwa maana ya kujaza mabeki watatu mbele ya washambuliaji wetu, kiukweli walituzidi kimbinu na kutufunga bao moja.

“ Prisons nao walicheza kwa kujiamini kama ilivyokuewa Lyon kwa kujaza mabeki nyuma golini kwao, lakini licha ya kuweka ulinzi huo mkubwa, tulitengeneza nafasi na kushindwa kuzitumia.

“Lakini hali hiyo haitufanyi tukate tamaa ya Ubingwa kwenye msimu huu, tunakwenda kujipanga kwa kukifanyia maboresho kikosi chetu na mzunguko wa pili tuendelee na kasi yetu,” alisema Mayanga.

Post a Comment

 
Top