WAKATI dirisha dogo la usajili wa soka Tanzania Bara likipangwa kufunguliwa Novemba 15, Simba imeelezwa kuwa na mkakati mzito wa kuhakikisha wanaimarisha safu yao ya ushambuliaji kwa kuiongezea makali kwa kumrejesha mshambuliaji wao kipenzi, Emmanuel Okwi.
Habari kutoka ndani ya uongozi wa Simba, ambao ni vinara wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, zinasema Okwi, anayekipiga katika Klabu ya SonderjykE ya Denmark, yuko tayari kurejea nchini na ameshafanya mazungumzo na ujumbe maalumu wa Simba uliokwenda nchini Denmark mwezi uliopita.
“Klabu ya SonderjykE imekubali kumuuza Okwi, naye amekubali kurejea Tanzania kuisaidia Simba kutwaa ubingwa, tunaamini mipango inakwenda vizuri sana, hivyo mashabiki wa Simba waendelee kuwa watulivu na kuwa wamoja na wenye mshikamano na timu,” alisema mtoa habari wetu.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Klabu ya SonderjykE imetaka kulipwa kiasi cha Dola 100,000 za Marekani, ambazo ni sawa na zaidi ya Sh milioni 200 za Tanzania, dau ambalo ndilo lilitumika kumsajili mshambuliaji Mzambia wa Yanga, Obrey Chirwa.
Katika timu ya SonderjykE, Okwi amekuwa hapati namba, ndiyo maana naye ameona bora arejee kwenye timu yake na viongozi wa Simba wanafanya kila linalowezekana ili kukamilisha zoezi hilo.
“Kila kitu kimekwenda vizuri na muda wowote kuanzia sasa atarejea kwao Uganda, kisha kuja Tanzania kuichezea Simba, suala la fedha za kumnunulia mchezaji huyo, mmoja wa matajiri wa timu hiyo kujitolea kutoa fedha hizo,” alisema.

Post a Comment

 
Top