WAPENZI wa Yanga wamekuwa katika kilio cha muda mrefu kutokana na kukosa kiungo mkabaji mwenye uwezo wa kuziunganisha vema safu za ulinzi na ushambuliaji, tatizo ambalo kwa sasa linakaribia kupata ufumbuzi kwani klabu hiyo inakaribia kumalizana na mafundi wawili wanaokipiga Mbeya City, Kenny Ally na Rafael Daud.
Ndani ya misimu mitatu iliyopita, Yanga imekuwa ikibahatisha katika nafasi ya kiungo wa kati ambapo imewatumia wachezaji zaidi ya sita ambao wote walishindwa kuitumikia nafasi hiyo ipasavyo.
Wachezaji waliowahi ‘kutupwa’ katika nafasi hiyo ni Said Juma Makapu, Salum Telela aliyetimkia Ndanda FC, Mbuyu Twite, Thaban Kamusoko ambaye kiasili ni kiungo mshambuliaji, Pato Ngonyani na Kelvin Yondani ambaye amekuwa akicheza kwa ufanisi zaidi kama beki wa kati.
Kwa kufahamu uzito wa tatizo hilo, Yanga iliamua kutupia macho kwingineko kuona kama inaweza kupata wachezaji sahihi wa kuitumikia nafasi hiyo na mwisho wa siku kuangukia kwa wakali hao wa Mbeya City.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa, baadhi ya vigogo wa Yanga hivi karibuni wametua mkoani Mbeya kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya kuwanasa wachezaji hao ambao kwa misimu minne sasa wamekuwa wakisakata kabumbu katika kikosi cha Wagonganyundo hao wa mkoani Mbeya.
“Kutokana na riporti iliyoandaliwa na benchi la ufundi chini ya kocha, Hans van de Pluijm, imehitaji kufanya usajili wa kutafuta beki wa kati ili kulimaliza tatizo lililokuwa likitusumbua kwa muda mrefu.
“Kufuatia ripoti hiyo, baadhi ya viongozi wamelazimika kutua mkoani Mbeya ili kufanya mazungumzo na wachezaji hao pamoja na mameneja wao na iwapo wakiweza kuafikiana, watavaa uzi kijani na njano kwenye mzunguko wa pili wa ligi,” alisema mtoa habari huyo.
BINGWA liliwasaka wanandinga hao ili kutaka kujua nini kinaendelea baina yao na mabingwa wa tetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo  Kenny alisema kuwa licha ya hadi sasa kutopokea taarifa yoyote kutoka kwa meneja wake juu ya kuhitajika Yanga , lakini yupo tayari kukipiga kwa mabingwa hao watetezi.
Alisema kwa sasa mkataba wake na Mbeya City umebakia miezi mitatu na ameshakaa nao mezani ili kuongeza mkataba, lakini ameshindwa kusaini  kutokana na kutokamilishiwa mahitaji yake muhimu aliyoyahitaji kutoka kwa Wagonga nyundo hao,
“Majukumu ya kuzungumza na timu yapo mikononi kwa meneja wangu,  lakini kwa upande wangu nipo tayari kwenda Yanga kuungana na Deus Kaseke, hivyo kama wananihitaji waje tutazungumza  kuhusu kiasi gani ninahitaji ili nikafanye nao kazi, nitakiweka wazi mara baada ya kuonana nao,” alisema kiungo huyo wa kati aliyewahi kukipiga Simba ‘B’ kabla ya kutua Mbeya City msimu wa 2013/14 kipindi kikosi hicho kikiwa chini ya kocha Juma Mwambusi ambaye kwa sasa ni msaidizi wa Yanga.
Wakati Kenny akisema hayo, kwa upande wa Rafael Duade amesema ili atue kwa Wanajangwani hao anahitaji dau la Sh milioni 30.
“Kwenda kucheza Yanga si tatizo kwangu ila wanatakiwa kutekeleza yale ninayoyahitaji kimkataba, kwani nitaondoka Mbeya City kwa milioni 30  na pia waende kuzungumza na mabosi wangu kwa kuwa nina mkataba wao wa mwaka mmoja, iwapo kama wataelewana Mbeya City na kutimiza ninachohitaji, nitaenda kufanya nao kazi pasipo na tatizo lolote,” alisema.

Post a Comment

 
Top