KOCHA wa Simba, Joseph Omog, anatarajiwa kuondoka leo Ijumaa
kwenda kwao Cameroon kwa ajili ya mapumziko lakini anaondoka akiwa tayari
ameshapanga mashambulizi kwa ajili ya raundi ya pili itakayoanza Desemba 17,
mwaka huu.
Omog anakwenda likizo akiiacha Simba kileleni mwa Ligi Kuu Bara ikiwa
na pointi 35, mbili zaidi ya Yanga, lakini pamoja na kuongoza ligi bado
amesisitiza kukiboresha kikosi chake na tayari amewasilisha pendekezo hilo kwa
mabosi wake, ripoti iliyojadiliwa Jumatatu na Jumanne wiki hii.
Omog alibainisha ripoti yake kusheheni vitu vingi vya kiufundi
lakini kwa tahadhari kubwa ya kutovuruga kikosi katika raundi ya pili.
Aina ya kikosi chake
Omog, 44, amesisitiza kuwa makini katika kupendekeza maboresho
kutokana na kikosi chake kuwa vizuri.
“Si kwamba najisifia, lakini utakubaliana nami kuwa mpaka sasa
tuna kikosi kizuri kinachofanya vizuri. Raundi ya kwanza tulikuwa na matokeo
bora, hivyo sikuona sababu ya kupangua kikosi, badala yake nimependekeza kuwe
na baadhi ya maboresho fulani kwa tahadhari ya kuivuruga timu,” alisema.
Apiga panga watatu
Licha ya tahadhari kubwa ya kutotaka kukivuruga kikosi lakini amebainisha
bado wapo wachezaji wanaoishi katika kivuli cha wenzao, hasa wazawa na
kupendekeza waachwe walau watatu.
“Pamoja na uzuri wa kikosi lakini kwenye ripoti nimebainisha kuna
baadhi nimeona hawana hadhi ama hawatufai kwa kipindi hiki tunapopigania
ubingwa. Sitasema ni kina nani lakini kuna wachezaji wengi wazawa wapo tu
hawana msaada kikosini, hivyo nimependekeza kati yao angalau watatu
waondolewe.”
Licha ya kutowataja, lakini orodha hiyo kwa vyovyote vile
itawagusa Awadh Juma, Abdi Banda, Malika Ndeule, Emmanuel Semwanza, Hija Ugando,
Peter Manyika, Denis Richard na Moussa Ndusha ambao umuhimu wao kikosini umeonekana
kuwa mdogo.
Post a Comment