KUMEKUCHA Jangwani! Huenda ukawa ni mwaka mwingine wa neema Yanga kutokana na kikosi hicho kusukwa vizuri kwa ajili ya mashindano.
Kwa taarifa ni kwamba kocha mpya aliyetua Jangwani, Mzambia George Lwandamina, ameanza kuisuka Yanga na sasa imethibitika kuwa ile injini ‘mwili jumba’ au kwa jina jingine ‘mkata umeme’ Justin Zulu, huenda akatua Yanga wakati wowote ndani ya wiki hii kwa ajili ya kumalizana na timu hiyo.
Yanga ilikuwa ikihitaji kiungo mmoja mkabaji mwenye uwezo mkubwa kutokana na nafasi hiyo kutokuwa na mtu wa uhakika na baada ya kushindwa kumpata Meshack Chaila wa Zesco ambaye inasemekana ana mkataba mrefu.
Inasemekana kuwa Zulu ndiye chaguo la kwanza la Lwandamina kutokana na uwezo wake mkubwa na huenda akachukua nafasi ya Mbuyu Twite ambaye kuna uwezekano mkubwa wa kuachwa.
Lwandamina |
Zulu ni raia wa Zambia ambaye ni mahiri sana akicheza kama kiungo mkabaji au wakati mwingine kiungo na ni stadi kwenye kufunga mabao ya mbali ambapo kwa sasa yupo kwenye kikosi cha Zesco ya Zambia alikotoka Lwandamina, ingawa hachezi kutokana na kufungiwa na Shirikisho la soka Ulimwenguni (Fifa).
Alifungiwa baada ya kuzinguana na wakala wake ambaye ni raia wa Misri baada ya yeye kugoma kumlipa wakala huyo wakati alipopata dili la kwenda Afrika Kusini hivi karibuni, ndipo wakala huyo akalalamika, Fifa ikamzuia mchezaji huyo kwa miezi sita.
Lakini habari zinasema Lwandamina amezungumza na wakala wake na wakakubaliana kwamba Yanga itamlipia deni analodaiwa ili akipige kwa wakali hao wa Jangwani.
Inaelezwa kuwa, uongozi wa Yanga uko tayari kumwaga fedha sasa kuhakikisha inaimarisha kikosi hicho kwa ajili ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Post a Comment