NOVEMBA 9, mwaka
huu Simba ilifungwa mabao 2-1 na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya
mfungaji wa Prisons akiwa Victor Hangaya. Sasa Simba inamtaka Hangaya.
Katika mchezo huo
wa Ligi Kuu Bara, Hangaya alifunga mabao yake dakika za 48 na 68 huku bao pekee
la Simba likifungwa na Jamal Mnyate dakika ya 41.
Mmoja wa mabosi
wa Kamati ya Usajili ya Simba, amesema wanamfuatilia Hangaya ili kukiongezea
nguvu kikosi chao hasa katika ushambuliaji kwani anaonekana yupo vizuri.
Katika ripoti
yake ya mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, Kocha wa Simba, Joseph Omog
amependekeza kusajili mshambuliaji, kipa na beki mmoja wa kati ili waweze
kufanya vizuri mzunguko wa pili.
“Hangaya ni mmoja wa washambuliaji wa kati
ambaye uongozi wetu unaangalia uwezekano wa kumsajili baada ya kocha
kupendekeza atafutiwe washambuliaji wawili wa kati na mazungumzo naye
yanaendelea,” alisema bosi huyo.
Hangaya alisema
kuwa: “Bado sijaonana uso kwa uso na viongozi wa Simba, lakini kuna baadhi yao
nimekuwa nikiwasiliana nao kwa simu na wanasema wanataka kunisajili.
“Kama wana nia ya
kweli, wanatakiwa kufuata tu utaratibu mimi nipo tayari kwa sababu soka ndiyo
maisha yangu kwani makataba wangu unaisha mwisho wa msimu huu.”
Katibu Mkuu wa
Simba, Patrick Kahemele alisema mambo yote ya usajili yakiwa tayari kila kitu
kitakuwa wazi.
Post a Comment