WAKATI mashabiki wa Yanga wakijawa na faraja baada ya kuenea kwa taarifa za chini kwa chini kuwa viongozi wao wanahaha kuinasa saini ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala,’ wenyewe Simba wameangua kicheko cha kebehi.
Taarifa za uhakika ambazo tumezipata zimedai kwamba, Yanga wanatafuta kila namna ya kumvuta beki huyo wa kushoto wa Simba, ambaye katika misimu hii kadhaa amekuwa kwenye kiwango bora.
Hii si mara ya kwanza Yanga kuhusishwa na kutaka saini ya beki huyo, lakini mara hii wamekuja kivingine, baada ya kutenga fungu kubwa ambalo bila shaka Simba wakifanya masihara watamkosa.
Taarifa za uhakika kutoka Yanga zinadai kuwa, mikakati ya kumng’oa Tshabalala inasukwa kwa ustadi wa hali ya juu na huenda ikatokea kama ilivyokuwa kwa Kelvin Yondani, aliyeondoka kiutani utani.
Hata hivyo, wakati hayo yakitokea, kwa upande wao Simba wamejibu mapigo na kuwaambia Yanga watasubiri sana, kwani beki huyo haendi kokote na kama wakimtaka itawabidi wavunje benki.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, alishaweka wazi kuwa beki huyo bado anao mkataba na pia wanafikiria kumuongeza mwingine na kuwataka mashabiki wao kutotishwa na taarifa hizo.
“Wanaodhani watamchukua kirahisi hivyo wanajidanganya, huyu bwana mdogo bado ana mkataba na Simba na kama kuna timu inamtaka itabidi wavunje benki, mimi sioni kwanini mashabiki wetu wanakuwa na wasiwasi juu ya jambo hilo ambalo haliwezekani,”  alisema.

Post a Comment

 
Top