WAKATI wachezaji wa Yanga wakipewa mapumziko baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kumalizika, straika wa kikosi hicho, Amis Tambwe, amesema hana muda wa kupumzika na badala yake anachukua mazoezi makali kwa lengo la kuisaidia timu yake.
Tambwe amesema, kwake haoni umuhimu wa kubweteka katika kipindi hiki ambacho timu yake ina kiu ya kutetea taji lake, lakini pia akihitaji tuzo ya mfungaji bora kwa mara ya tatu.
“Eti nipumzike! Naanzeje kufanya hivyo, nina kiu ya kuiona Yanga ikitetea ubingwa wake kwa mara nyingine msimu huu, lakini pia mimi niweze kuibuka mfungaji bora kwa mara ya tatu na kuweka historia ya kipekee katika soka la Tanzania.
“Ratiba yangu kwa siku ni sawa na ile ya Yanga tu, kwani asubuhi nafanya mazoezi na inategemea kama nikienda gym basi jioni nitafanya mazoezi ya kucheza mpira, kwa ufupi sitaki kulala hivihivi,”alisema.
Katika msimamo wa ufungaji bora, Tambwe, ambaye ni mfungaji bora wa ligi msimu uliopita baada ya kufunga mabao 21, hivi sasa ameshaifungia timu yake mabao saba na kushika nafasi ya pili nyuma ya Shiza Kichuya wa Simba, anayeongoza akiwa na mabao tisa.
Post a Comment