MIONGONI mwa mijadala inayoendelea hivi sasa kwa wanachama
na mashabiki wa klabu ya Simba, kufuatia kupoteza michezo mwili ya mwisho ya
Ligi Kuu ya Vodacom Bara mzunguko wa kwanza, ni pamoja na udhaifu wa kipa namba
moja wa kikosi hicho, Vicent Angban.
Angban, raia wa Ivory Coast, anatajwa kuonyesha kiwango
kibovu katika mechi hizo na kusababisha timu yake kuchapwa kwa bao 1-0 na timu
ya African Lyon, kabla ya kutandikwa tena 2-1 katika mechi ya funga dimba,
dhidi ya Prisons ya Mbeya, iliyochezwa Jumatano iliyopita.
Kufuatia mapungufu hayo, kocha wa makipa wa Wekundu hao wa
Msimbazi, Adam Abdallah, maarufu kama
‘Meja Luu’, ameweka bayana majina ya makipa ambao anaamini kama
watakuwemo katika kikosi chao katika mzunguko ujao, basi lango lao halitakuwa
na madhara.
Amewataja makipa hao kuwa ni raia wa Uganda Frank Muhonge,
anayekipiga katika Klabu ya Stand United ya Shinyanga na Youthe Rostand, ambaye
ni raia wa Cameroon, anayechezea klabu ya African Lyon.
Amewaelezea makipa hawa wana utulivu wanapokuwa golini na
vilevile wanaonyesha kumudu mikiki mikiki pale timu yao inapocheza na kikosi
chenye washambuliaji wenye kasi.
Hata hivyo, amemtetea Angban, licha ya kudaiwa kupungua
uwezo wake, lakini bado alihitaji kupumzika kutokana na kucheza mechi zote 15
katika ligi hiyo tangu ilipoanza.
Kuhusu kipa namba mbili wa Simba, Manyika Peter, alisema
bado anaweza kuwa na manufaa kwa timu, lakini kitendo cha kumuweka benchi kwa
kipindi kirefu kimemtoa nje ya mchezo.
Licha ya majina hayo, Wekundu hao wa Msimbazi pia wanamtaja
kipa Abbas Pira, aliyewahi kuchezea klabu mbalimbani nchini Uingereza, ambaye
ameonyesha nia ya kujiunga na klabu hiyo, endapo atafikia makubaliano na
uongozi.
Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, alikataa kuzungumzia suala
lolote la kuacha au kusajili mchezaji kwa kipindi hiki, akidai kwamba hilo ni
jukumu la kamati ya usajili, ambayo itafanya kazi na kisha kuwasilisha ripoti
kwake na hivyo yeye kuyafanyia kazi.
Simba imemaliza mzunguko wa kwanza wa michuano ya Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, ikiwa kileleni kwa kujikusanyia jumla ya
pointi 35, baada ya kucheza michezo 15, ikishinda 11, kutoa sare michezo miwili
na kupoteza miwili.
Post a Comment