LICHA ya kuaga
kuondoka, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm amegoma kumpisha George
Lwandamina katika ardhi ya Bongo na ameweka wazi kuwa bado yupo sana nchini
akiwa na mkewe kwa ajili ya kupumzisha akili yake.
Kocha huyo,
Jumanne iliyopita katika mazoezi ya mwisho ya kujiandaa na mechi dhidi ya Ruvu
Shooting aliwaaga wachezaji wa timu hiyo huku nafasi yake ikichukuliwa na
Mzambia, George Lwandamina ambaye yupo nchini tangu Jumatano iliyopita na
ameshasaini mkataba wa miaka miwili kimyakimya huku viongozi wakiendelea
kuwazuga wanachama kwa kukana hadi pale watakapokuwa tayari kumtambulisha.
Mholanzi huyo,
mechi dhidi ya Ruvu ilikuwa ya mwisho kwake kukaa kwenye benchi na kufanikiwa
kupata ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na
Championi Jumatatu, Pluijm alisema haoni sababu ya kuondoka hivi sasa kutokana
na mke wake kuwepo nchini wiki ya pili sasa akitokea nyumbani kwao Ghana
wanapoishi.
Pluijm alisema
mwaka huu hawakupata nafasi ya kupumzika na familia zao kutokana na kubanwa na
michuano ya kimataifa iliyokwenda sambamba na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara,
hivyo amepanga kupumzisha akili yake hapa nchini kwa kula bata na mke wake.
“Kama
ulivyokuwa unaona ratiba ilivyokuwa inatubana mwaka jana na huu, tulikosa muda
wa kupumzika kabisa tofauti na timu nyingine kutokana majukumu ya michuano ya
kimataifa.
“Hivyo, huu ni
muda muafaka kwangu kupumzisha akili na kufurahia maisha na mke wangu ambaye
amekuja tangu wiki iliyopita, hivyo nipo naye nchini kwa ajili ya mapumziko
huku nikiweka sawa mambo yangu binafsi,” alisema Pluijm.
Post a Comment