YANGA huenda kesho Jumapili isimtumie
beki wake wa kulia, Hassan Kessy baada ya jana Ijumaa kushindwa kumaliza
mazoezi ya timu yake baada ya kupata maumivu ya mgongo na kuzua hofu ya
kutocheza mechi dhidi ya Prisons.
Prisons iliyo katika nafasi ya tisa na
pointi zake 16 katika Ligi Kuu Bara, kesho itacheza na Yanga kwenye Uwanja wa
Sokoine katika muendelezo wa ligi hiyo.
Katika mazoezi ya Yanga jana Ijumaa
asubuhi kwenye Uwanja wa Sokoine, Kessy alishindwa kumaliza mazoezi hayo na
kuzua hofu ya kukosa mechi dhidi ya Prisons.
Kessy hucheza beki ya kulia
akipokezana na Juma Abdul ambaye sasa ni majeruhi wa maumivu ya kiuno na
misuli, hivyo nafasi hiyo kama Kessy hatokuwepo atacheza mchezaji kiraka ambaye
ni Mbuyu Twite.
Daktari wa Yanga, Edward Bavu
aliliambia Championi Jumamosi kuwa: “Kessy amepata mshituko mgongoni ndiyo
maana hajaendelea na mazoezi, sitegemi kuona akikosa mechi na Prisons japokuwa
itategemea na hali yake.”
Kwa upande wake, Kocha wa Yanga, Hans
van Der Pluijm akizungumzia hali hiyo ya Kessy alisema: “Ni maumivu madogo, ila
bado ana muda wa mazoezi tutamsikiliza daktari kuhusu hali yake halafu ndipo
tutamtumia.”
Post a Comment