Ariana Yohana
BAADA ya kuwa kwenye mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa za kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Dunia, sasa utamu wa ligi kubwa za Ulaya umerejea, wikiendi hii ni moto juu ya moto.
Hispania ‘La Liga’ kutakuwa na mtanange wa kukata na shoka kati ya wenyeji Atletico dhidi ya Miamba ya Bernabeu, Real Madrid acha huko pia kule Ujerumani ‘Bundesliga’ Dortmund yenyewe itakuwa uwanjani kuonyeshana kazi na Bayern Munich.
Siyo hizo tu, leo pia kutakuwa na mechi ya wanaojua wengine, Man United ambao watakuwa Old Trafford kuwakaribisha washika mtutu wa Gunners, Arsenal mechi ambayo inatarajiwa kuwa kali zaidi.
Lakini pia kesho kutakuwa na mechi kati ya AC Milan na Inter Milan za kule Serie A, Italia.
Hapa leo tunaangalia kikosi bora kinachoundwa na nyota kutoka Man U na Arsenal msimu huu yaani 2016/17.

KIPA: David De Gea
Kipa Petr Cech wala hakufanya uzembe wowote mpaka sasa msimu huu lakini ukiangalia kati ya makipa bora ulimwenguni yeye hana kitu spesho zaidi cha kumfanya awe bora au awepo kwenye listi ya makipa wakali. De Gea anaingia kuwa kipa namba moja kutokana na uwezo wake, kwa maana ya kuokoa michomo mingi zaidi licha ya kuwa amefungwa magoli mengi zaidi ya Cech. Amefanya kazi kubwa msimu huu mpaka sasa na hiki ndicho kinamfanya asimame namba moja mbele ya Cech.


Beki wa kulia: Ashley Young
Young ameingia hapa kutokana na mlinzi wa Arsenal, Hector Bellerin kuwa na majeraha ya muda mrefu. Pia hata Antonio Valencia hawezi kukaa hapa kwa kuwa hakushiriki mechi nyingi kutokana na kuwa majeruhi.

Beki wa kati: Laurent Koscielny
Wala hakuna ‘dauti’ kuhusu huyu bwana kuwa hapa, Mfaransa huyu ameuanza msimu vyema sana akitengeneza pacha bora na mwenzake,  Shkodran Mustafi. Amefanya kazi kubwa sana. Eric Bailly wa Man U ambaye naye anacheza nafasi hii ameshindwa kuingia hapa kutokana na kutocheza mechi nyingi kutokana na kukumbwa na majeruha.

Beki wa kati: Shkodran Mustafi
Mustafi ameingia tu msimu huu pale Arsenal na kupata nafasi moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza na hiyo yote ni kutokana na kuwa mtu wa kazi. Ametengeneza pacha nzuri na besti yake, Koscielny.


Beki wa kushoto: Nacho Monreal
United wamekuwa wakiwachezesha wachezaji tofautitofauti katika nafasi ya ulinzi wa kushoto na hiyo imesababisha kushindwa kupata nafasi hapa. Monreal, amekuwa akionyesha uwezo mkubwa japokuwa awali wakati anajiunga na Arsenal ilimchukua muda kukopi mfumo wa Arsene Wenger. Nyota wa United ambao huwa wanachezeshwa pembeni ni kama Daley Blind, Luke Shaw na Matteo Darmian.

Kiungo mkabaji: Michael Carrick
Carrick ameonekana kuwazidi Francis Coquelin na Granit Xhaka. Carrick ni mchezaji muhimu pale Red Devils na akiwa hapo hucheza vizuri.

Kiungo wa kati: Paul Pogba
Baada ya kufanikiwa kurejea United kwa mara ya pili, Pogba alionekana kuhitaji muda kidogo ili akopi mfumo wa Kocha Jose Mourinho. Alionyesha kiwango kikubwa kwenye mchezo dhidi ya Swansea, mshindani wake hapa alikuwa ni Santi Cazorla ambaye amekuwa nje kwa muda kutokana na kusumbuliwa na majeraha.

Kiungo mshambuliaji: Mesut Ozil
Wayne Rooney alicheza vizuri sana kwenye mechi dhidi ya Swansea lakini hiyo haiwezi kumfanya achukue nafasi hii mbele ya Mjerumani Mesut Ozil. Ukiachana na ubora wa pasi zake lakini pia Ozil anafunga mabao.


Winga wa kushoto: Alexis Sanchez
Mchile huyu amekuwa akiwafanya wadau wajiulize kama leo atacheza hiyo nyote ni kutokana na majeraha aliyolipotiwa kuyapata alipokuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa hata hivyo katika mchezo wa mwisho alicheza na akafunga mabao mawili dhidi ya Uruguay. Hata msimu uliopita wakatai Arsenal ikishinda mabao 3-0 dhidi ya United alionekana kuitikisa vilivyo safu yao ya ulinzi.

Winga wa kulia: Theo Walcott
Ameonekana kuanza msimu huu kwa kasi, mpaka sasa kafunga mabao matano huku pia akitengeneza nafasi mbalimbali za kufunga. Mourinho ana wachezaji wengi ambao wanacheza nafasi kama hii lakini ukiwalinganisha na Walctott ‘dogo’ anaonekana kuwafunika.

Mshambuliaji: Marcus Rashford
"Tusisahau mwaka uliopita, kijana aliyetumaliza ni Rashford.” Alisema Kocha wenger alipokuwa akimzungumzia kijana huyo mdogo. Kwa kuwa Zlatan Ibrahimovic anatumikia adhabu ya kadi na leo hatocheza, hivyo nafasi itakuwa kwa Rashford kuwaongoza wenzake kushambulia.

Post a Comment

 
Top