JUZI Alhamisi Yanga iliifunga Ruvu Shooting mabao 2-1 katika Ligi Kuu Bara huku nahodha wa timu hiyo Haruna Niyonzima akiwa nyota wa mchezo, lakini gumzo ni chenga yake aliyompiga beki Mao Bofu.
Niyonzima, raia wa Rwanda, alitoa pasi ya bao dakika ya 31 na Simon Msuva akafunga lakini naye akafunga dakika ya 56 baada ya kupokea pasi ya Donald Ngoma na kuipa ushindi timu yake.
Pasi ya bao la Msuva ilionekana kuzua gumzo kwa wadau wa soka waliokuwepo uwanjani hapo na wale waliokuwa wakifuatilia mchezo huo runingani hasa chenga ambayo Niyonzima alimpiga Bofu kabla ya kutoa pasi.
Niyonzima alikokota mpira akiwa upande wa kulia wa uwanja jirani na lango la Ruvu Shooting kisha akampiga chenga kali Bofu na kutoa pasi kwa Msuva aliyefunga.
Akizungumzia chenga hiyo ambayo video yake imesambaa katika mitandao ya kijamii, Niyonzima alisema ana aina nyingi za chenga ambazo zote zinatokea kutokana na muda husika kama aliyompiga Bofu.

“Nimepanga kuonyesha kiwango changu kile nilichokuwa nacho awali, ninataka kurejesha heshima yangu, wengi wameiona chenga hii ya mechi na Ruvu, lakini nimepiga chenga nyingi tangu niliporudi kikosini.
“Mabeki wengi wa ligi kuu wanatumia nguvu nyingi kuliko akili, hata wale wa Ruvu walitumia nguvu sana kutuzuia, yule jamaa ilikuwa ni lazima aanguke kutokana na chenga niliyompiga,” alisema Niyonzima.
Niyonzima akiwa na mpira alichanganya miguu na kumchanganya Bofu ambaye alianguka akiwa katika harakati za kumzuia kiungo huyo.

Post a Comment

 
Top