MAMBO sasa hadharani, baada ya kocha mpya wa Yanga, George Lwandamina, kuchambua uwezo wa kila mchezaji wa timu hiyo, kabla ya kuanza rasmi kuifundisha kwa ajili ya Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa.
Lwandamina ambaye tayari yuko nchini, ameangalia mikanda ya video katika mechi mbalimbali walizocheza wachezaji hao na kuridhishwa na viwango vya baadhi yao.
Taarifa ambazo BINGWA limezipata kutoka ndani ya Yanga, zinasema baada ya kocha huyo kuitupia jicho mikanda aliyokabidhiwa, amefanikiwa kumchambua mchezaji mmoja mmoja, huku akionyesha kufurahishwa na uwezo wa winga, Simon Msuva.
Lwandamina amemwelezea Msuva ni mchezaji mwenye uwezo wa hali ya juu, ingawa ana matatizo madogo madogo ambayo anaweza kumrekebisha na kuwa tishio zaidi katika kikosi chake.
Pamoja na sifa hizo kwa Msuva, kocha huyo ameonekana kuwakubali wachezaji wawili wa kimataifa, ambao ni Mzambia mwenzake Obrey Chirwa na Amissi Tambwe.
“Kocha anasema, Chirwa anamfahamu tangu akiwa timu za taifa za vijana za Zambia na kwamba yeye ni winga na si mshambuliaji, hivyo amemuona anachezeshwa kama mshambuliaji, jambo ambalo si sahihi,” kilisema chanzo chetu.
Lwandamina amemwelezea Chirwa kuwa ni mchezaji mzuri aliyekuwa akichezeshwa winga katika kikosi cha timu ya vijana ya Zambia iliyokuwa chini ya miaka 20.
Kocha huyo ambaye anatarajia kuanza kibarua chake hivi karibuni baada ya timu kurejea kutoka mapumziko, pia amemwelezea Tambwe kama mshambuliaji kwenye uwezo hivyo hana sababu ya kusajili mshambuliaji mwingine au kumleta Jesse Were kama alivyofikiria.
Kutokana na uwezo aliouonyesha Tambwe katika mechi mbalimbali, ataendelea kumpa nafasi katika kikosi chake huku akiendelea kukisuka upya. http://spotiripota.blogspot.com/
Lwandamina amewadokeza Wanayanga kuwa katika nafasi ya ulinzi amewakubali Vincent Bossou na Andrew Vincent ‘Dante’, lakini akishindwa kuwazungumzia mabeki wa pembeni, Haji Mwinyi, Juma Abdul, Oscar Joshua na Hassan Ramadhani ‘Kessy’.
Pamoja na kumkubali Bossou, lakini anadaiwa anatarajia kuachana na timu hiyo na kwenda kujiunga na Zamalek ya Misri.
Lakini Lwandamina ameshindwa kumzungumzia kwa kina Donald Ngoma ambaye inadaiwa amepata ofa ya kwenda kucheza katika klabu ya Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini. http://spotiripota.blogspot.com/
Hata hivyo, Lwandamina ameahidi kumleta kiungo mkabaji baada ya kuona upungufu mkubwa katika idara hiyo.
Katika hatua nyingine, Lwandamina alimuulizia kiungo mkabaji wa timu hiyo, Salum Telela, aliyetemana na klabu hiyo katika msimu huu, ambaye kwa sasa anakipiga Ndanda.
Lwandamina alimuliza kiungo huyo, baada ya kushindwa kumwona katika vikosi alivyoangalia katika mikanda ya video aliyopatiwa akimwamini ni mchezaji mzuri.
“Alimwona Telela katika moja ya mikanda, lakini hakumwona kwenye mikanda mingine, alipoulizwa aliwaambia huyo ameondoka, kwa kweli amevutiwa naye sana na huenda akaomba arudishwe licha ya kwamba uongozi ulimtema kutokana na suala la kinidhamu,” kilisema chanzo chetu. http://spotiripota.blogspot.com/
Telela alicheza vizuri katika michuano ya kimataifa msimu uliopita na pengine kumvutia Lwandamina aliyeamini angemkuta Jangwani.
Lwandamina anatarajiwa kuanza kazi ya kuifundisha Yanga Novemba 28, mwaka huu baada ya Hans van der Pluijm kupewa majukumu mengine ya kiutawala.
Post a Comment